Katibu Mkuu kiongozi ataka ongezeko la gawio kwa Serikali

Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka amewapa changamoto wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo Serikali ina hisa chache kuangalia namna wanavyoweza kuongeza ufanisi na gawio kwa Serikali.

Dk Kusiluka ametoa rai hiyo usiku wa jana Machi 28, 2025 katika hafla ya kufunga mafunzo ya siku tatu ya wakurugenzi wa bodi za kampuni ambazo Serikali inaumiliki wa hisa chache yaliyofanyika Kibaha mkoani Pwani.

Alitoa wito huo wakati ambao takwimu za Ofisi ya Msajili wa Hazina zinaonyesha kuwa katika mwaka wa fedha uliopita, Serikali ilipata gawio la Sh195 bilioni kutoka kampuni hizi limeongezeka kwa kutoka Sh58 bilioni mwaka 2019/20.

“Ninaamini mwaka ujao wa fedha nitaona gawio kutoka taasisi mnazosimamia likiongezeka. Hilo ninawaachia kila mmoja kwa nafasi yake akazingatie hili. Mafanikio yetu yataakisi juhudi za Serikali ambazo zimekuwa zikifanyika za kuweka mazingira rafiki na wezeshi ya biashara,” amesema Dk Kusiluka.

Mbali na ongezeko la gawio pia amezitaka kampuni hizo kuongeza kiwango chake rudisho la uwekezaji ‘return on investment’ kutoka asilimia saba ya sasa hadi kufikia zaidi ya 10 mwaka ujao wa fedha.

 “Hii pia ni changamoto, angalieni namna ya kukuza rudisho la uwekezaji kutoka asilimia saba ya sasa kwenda zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka na ili kufikia azma hii mnapaswa kuongeza ufanisi wa utendaji,” amesema.

Ofisi ya Msajili wa Hazina inasimamia jumla ya taasisi 308 ambapo kati ya hizo 56 ni zile ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache.

Katika taasisi hizo serikali imefanya jumla ya uwekezaji wa Sh86.3 trilioni na kati ya kiasi hicho Sh2.9 trilioni zikiwekezwa kwenye kampuni ambazo serikali ina umiliki wa hisa chache na Sh83.4 trilioni kikienda kwa taasisi ambazo serikali ina umiliki wa asilimia 100.  

Dk Kusiluka pia alitumia nafasi hiyo kuzungumzia mwongozo ulioboreshwa wa wakurugenzi wa Bodi wa Hisa chache uliozinduliwa Jumatano wiki iliyoisha wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere.

“Nimeupitia kwa kina na nimeona umejaa maelekezo mazuri yatakayotusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa weledi na kwa wakati ni katika muktadha huo ninawaelekeza wakurugenzi wa bodi kuutumia kikamilifu ili kuongeza ufanisi katika maeneo yenu,” amesema.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu amewataka wawakilishi wa Serikali kwenye bodi za kampuni huzo kupeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Aliwataka wawakilishi hao ambao ni wakurugenzi wa bodi kuzitendee haki nafasi walizopewa ili kuhakikisha kuwa serikali inanufaika na uwekezaji iliofanya kwenye kampuni ambazo ina umiliki wa hisa chache.

“Nyie ni jicho la serikali hivyo mnapaswa kutokuchukulia kiwepesi nafasi mlizopewa, vinginevyo mtakuwa hamuitendei haki Serikali na Watanzania wote kwa ujumla. Lazima mjidhatiti na kama unaona hauko kwenye nafasi ya kufanya hivyo kutokana na kutokuwa na muda wa kutosha, ni vyema ukasema ili nafasi hiyo wapewe wengine,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *