Katekista, wengine watatu wahofiwa kufa maji Ziwa Victoria

Musoma. Miili ya watu watatu wanaohofiwa kufariki dunia baada ya kuzama ndani ya Ziwa Victoria katika kisiwa cha Rukuba wilayani Musoma bado haijapatikana.

Watu hao akiwamo Katekista wa Kanisa Katoliki Parokia Teule ya Rukuba Jimbo Katoliki la Musoma mkoani Mara, Cleophace Mganga (45) wanahofiwa kufariki dunia baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia kuvua dagaa kupigwa na dhoruba, kisha kuzama usiku wa Aprili 21, 2025.

Wengine wanaohofiwa kufariki dunia ni pamoja na Frederick Ibaso (39) na Revocatus Ntega (35).

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatano, Aprili 23, 2024, Mwenyekiti wa Kijiji cha Rukuba, Jafari Kibasa amesema utafutaji unaendelea, ingawa hadi sasa hakuna mtu aliyepatikana.

Hata hivyo, amesema kwa  uzoefu walionao miili ya watu hao itaanza kuibuka baada ya siku tatu tangu kutokea kwa tukio hilo.

“Hapa ingawa utafutaji unaendelea, sisi tunajua miili itaanza kuibuka yenyewe kuanzia siku ya tatu, kwa hiyo tunategemea kuanzia kesho, ingawa hadi sasa kuna watu kule lilipotokea tukio wanaendelea na utafutaji,” amesema.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema utafutaji wa watu hao unaendelea, ingawa matumaini ya kuwapata wakiwa hai ni madogo kwa sasa.

“Hadi sasa hakuna taarifa mpya, tunaendelea kuwatafuta kwa kushirikiana na wananchi wa kule,” amesema Magere.

Tukio hilo liliwahusisha watu wanne ambao ni wavuvi wa dagaa, baada ya mtumbwi kuzama, mmoja kufanikiwa kuogelea na kukaa kwenye boya lililotengezwa kwa matete kabla ya kupata msaada kutoka kwa wavuvi wengine.

Kamanda Magere amemtaja aliyenusurika katika tukio hilo ni Makebe Buriro (22) aliyeokolewa na wavuvi wengine baada ya kuelea na boya hilo kwa muda ziwani humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *