
KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amesema licha ya timu hiyo kuwa na hali mbya, lakini tayari amekaa na wachezaji ili kupambana kwa mechi zilizobaki na kujinusuru wasishuke daraja.
Kaseja amekabidhiwa timu baada ya Melis Medo kutemwa na kuibukia Singida Black Stars akiajiriwa katika nafasi ya kocha msaidizi, alisema kwa mechi zilizosalia bado wana nafasi ya kusahihisha makosa.
“Bado tuna nafasi ya kufanya vizuri naanza na mechi mbili nyumbani, hii ni nzuri kwangu hata kwa wachezaji pia tunatakiwa kutumia vizuri uwanja wetu na kupata pointi zote sita japo haitakuwa rahisi lakini ili kuwa bora ni kufanya vizuri nyumbani,” alisema Kaseja na kuongeza;
“Kwa sasa tunaendelea vizuri na mazoezi kujiweka tayari kwa mchezo wetu dhidi ya Pamba Jiji nyumbani, hautakuwa rahisi tunakutana na timu ambayo imeimarika na ipo katika harakati ya kupambania nafasi ya kucheza ligi msimu ujao kama ilivyo upande wetu.”
Kaseja alisema mikakati ni kupata matokeo katika mechi za nyumbani ikiwamo dhidi ya Coastal Union ili kuwarudisha wachezaji kwenye morali nzuri na baada ya hapo kupambana na mechi nyingine nje ya Kaitaba huku akiweka wazi kuwa hakuna kinachoshindikana.
“Nimewajenga wachezaji wangu kuwa pamoja na kuwa kwenye nafasi mbaya bado tunaweza kuwa bora na kucheza ligi msimu ujao kwani tukishinda mechi mbili ni pointi sita tunapanda nafasi moja au zaidi itategemea na idadi ya mabao ya kufunga,” alisema.
“Wachezaji waliopo wana uwezo wa kupambana na ni wazoefu wa ligi kama tutaweza kufikia malengo tuliyojiwekea hakuna kitakachotukwamisha kucheza tena ligi msimu ujao japo sio rahisi tunatakiwa kupambana sana.”
Kagera ipo nafasi ya 15, ikiwa na pointi 16 baada ya mechi 22, ikishinda michezo mitatu, sare saba na kupoteza 12, ikifunga mabao 16 na kufungwa 30 na sasa imesaliwa na mechi nane kufunga msimu.