​​​​​​​Kariakoo yafurika kuelekea Sikukuu ya Eid, abaya zapanda bei

Dar es Salaam. Siku chache kabla ya waumini wa dini ya Kiislamu kusherehekea sikukuu ya Eid, mitaa ya Kariakoo imefurika watu leo Machi 29, 2025 waliofuata mahitaji mbalimbali.

Katika mitaa kumekuwa na msongamano wa watu, magari na bidhaa zilizopangwa kando mwa barabara, watoto wakijikuta katika hali ngumu.

Kwenye mitaa ya Msimbazi, Congo, Mkunguni, Sikukuu, Nyamwezi na Uhuru, baadhi ya wazazi na walezi waliofuatana na watoto wamekuwa wakipita kwenye maduka na vibanda kununua nguo na viatu.

Salma Hamisi, mama wa watoto wawili aliyetoka Mbagala wilayani Temeke, anasema: “Mwaka jana bei zilikuwa tofauti kabisa, tulinunua magauni ya watoto kwa Sh25,000 lakini sasa ni Sh30,000 na kuendelea. Viatu navyo vimepanda, lakini siwezi kuacha watoto wangu wakose furaha ya Eid,” amesema Salma akiwa ameshika mifuko miwili yenye mavazi aliyowanunulia watoto wake katika Mtaa wa Congo.

Miongoni mwa nguo zilizopanda bei ni abaya kwa ajili ya wanawake ambazo za kawaida ziliuzwa kuanzia Sh30,000 awali lakini kuanzia Machi 28, 2025 zinauzwa Sh35,000 hadi Sh60,000. Kwa zenye urembo na nakshi zaidi zikiuzwa hadi Sh130,000. Si kwa abaya pekee, bei zimepanda hata kwa madera na vijora.

“Huu ni wakati wa watoto, sisi wazazi tunaweza kuvaa za mwaka jana,” amesema Jamila Said, akiwa na watoto wake watatu wakichagua nguo katika Mtaa wa Narung’ombe.

Licha ya mvua kunyesha kuanzia alfajiri kabla ya kukatika baadaye mchana, eneo la Kariakoo kumekuwa na hali ya joto kutokana na msongamano.

Joto liliongezeka ndani ya maduka katika Mtaa wa Raha baada ya umeme kukatika tangu saa sita mchana.

Wengi walioonekana kwenye mitaa ya Kariakoo ni wanawake, baadhi wakiwa wamebeba watoto mgongoni, wengine wakishikwa mikono.

“Msongamano huu ni wa kila mwaka, lakini hatuna namna. Tunajua tutaumia na tutakanyagana, lakini tukifika nyumbani watoto wakivaa nguo mpya na kucheza kwa furaha, tunasahau tabu zote,” amesema Mohamed Rashid, baba wa watoto wawili aliyekuwa Mtaa wa Nyamwezi akinunua kanzu kwa ajili ya mtoto wake.

Wachuuzi nao wanapita huku na huko wakinadi bidhaa za nguo, viatu na mapambo.

“Haya twende kazi tuvae abaya na vijora bila kumsahau mwanao nguo Sh6,000 twende kazi mama penda mwanao akatambie wenziwe mtaani,” ndivyo alivyonadi bidhaa Athumani Salehe, katika Mtaa wa Raha.

Katika msongamano huo, baadhi si wanunuzi wa bidhaa bali wamewasindikiza wenzao kununua mahitaji kama anavyoeleza Amina Sheria mfanyabiashara wa madera:

“Unakuta wameongezana wanne unawakaribisha wanachagua, anatokea mmoja anasema hiyo mbaya tuondoke, hawa wanatuharibia biashara badala ya kuacha mtu aamue wao wana kazi ya kuponda alichopenda mwenzao.”

Mchuuzi wa nguo za kiume, Peter Selem amesema kwa upande wake biashara si nzuri.

“Wanaofika dukani ni wachache wateja ninaopata ni walewale wanaokuja kuchukua mzigo wa jumla na wanaotoka nje ya Tanzania tofauti na matarajio yangu nilijua nitaongeza wateja wapya kipindi hiki,” amesema.

Maduka ya viungo

Katika maandalizi ya sikukuu, maduka yanayouza viungo kwenye Mtaa wa Tandamti na Sikukuu kumekuwa na umati.

“Nimekuja kununua viungo Karikaoo kwa sababu ni vizuri na si vya kukaa dukani muda mrefu, bei yake ni nafuu tofauti na masoko mengine ndiyo maana nipo hapa navumilia foleni ili nipate kilicho bora,” amesema Hadija Seif, mkazi wa Upanga.

Msongamano wa magari

Barabara za Msimbazi na Uhuru zimekuwa na msongamano wa magari sawa na barabara ya Mafia, hivyo watu kulazimiaka kukaa barabarani kwa zaidi ya saa moja kabla ya kufika waendako.

Hali ikiwa hivyo, bodaboda na bajaji zimekuwa zikipenya kila zinapopata upenyo hivyo kuhatarisha usalama wa watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *