Kariakoo Dabi yawapa kigugumizi makocha Yanga, Simba

Katika kile kinachoonekana ni kupanda kwa homa ya mechi ya watani wa jadi wa Kariakoo ‘Kariakoo Dabi baina ya Yanga na Simba kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, makocha wa timu hizo kila mmoja ameshindwa kuitabiria timu yake ushindi.

Wakizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari leo, kocha Miloud Hamdi wa Yanga na Fadlu Davids wa Simba, kila mmoja ametabiri mechi hiyo kuwa ngumu.

 Hamdi amesema kuwa anaamini mechi hiyo itakuwa bora nzuri na timu itakayokuwa na mbinu bora zaidi itapata ushindi.

“Ni jambo la kipekee kucheza ‘dabi’. Sio ‘dabi’ yangu ya kwanza lakini hii ni miongoni mwa ‘dabi’ tano bora Afrika na hata kwa wachezaji ni jambo la kipekee.

“Mechi ya kesho ni ya aina yake. Ni tofauti na mechi nyingine hivyo tumejiandaa vizuri na nimekuwa na siku tano za kuwaandaa wachezaji na kila kinachohitajika kufanywa na benchi langu la ufundi kimefanyika.

“Nategemea mechi ya kesho mchezo wa soka kushinda. Tunaiheshimu Simba na tunaheshimu mashabiki wake lakini sisi ni Yanga. Wao wana safu bora ya ulinzi na sisi tuna safu bora ya ushambuliaji hivyo naamini itakuwa ni mechi bora kimbinu. Natumaini mechi itakuwa ya wazi na tunahitajika kuwa bora zaidi kimbinu,” amesema Hamdi.

Hamdi amesema kuwa ana imani uwezo wa wachezaji wake utaamua mechi huku akifichua kuwa mchezaji aliye katika hatihati ya kucheza ni Stephane Aziz Ki kutokana na maumivu.

“Sina presha na ninajiamini na wachezaji wangu. Kwa nini niwe na hofu na sisi Yanga ni timu kubwa? Nina uhakika watatoa kila walichonacho kwa ajili ya mashabiki.

“Tuna mchezaji mmoja tu ambaye hayuko sawa naye ni Aziz Ki. Amekuwa na matibabu wiki nzima kwa hiyo kwa kesho ni hamsini hamsini lakini wachezaji wengine wote wako tayari,” amesema Hamdi.

Kocha wa Simba, Fadlu Davids amesema timu yake itamkosa Mzamiru Yassin huku kipa Moussa Camara na beki Che Malone Fondoh wakisubiri vipimo vya mwisho kujua utayari wao wa kucheza.

“Maandalizi yetu yameenda vizuri tukijua ni wiki ya ‘dabi’. Kumekuwa na mvuto katika mazoezi na kila mchezaji anaonekana anatamani kucheza mechi hii. Mzamiru atakuwa nje na majeruhi na tutakuwa na tathmini ya mwisho ya majeraha ya Che Malone na Camara kuona uwezekano wao wa kucheza.

 “Dabi ya kwanza ni tofauti na hii ya sasa. Tulikuwa na umiliki wa muda mrefu wa mpira bila shaka tulikuwa timu bora. Tunatakiwa kuwaheshimu. Yanga ina wachezaji wengi wazuri mmojammoja, tunaamini dondoo ndogondogo ndizo zitaamua mchezo,” amesema Fadlu.

Kocha huyo ameongeza kuwa Simba inafahamu ukubwa na umuhimu wa mechi hiyo.

 “Ni mechi kubwa ambayo tunaenda kuikabili. Na ina nafasi kubwa ya kuamua ubingwa. Tunatakiwa kufanya kwa ajili ya mashabiki wetu. Hatujafanya vizuri katika dabi zilizopita na wachezaji wetu wanafahamu hilo.

 “Tunatakiwa kuwa makini sana. Kuangalia maeneo gani tutapasia na wapi hatutopasia. Tumejifunza kutokana na makosa yaliyopita na nina imani hayatojirudia,” amesema Davids.