Wkiendi iliyopita ya Machi 8, 2025 stori kubwa nchini ilikuwa ni tukio la kuahirishwa kwa mchezo wa dabi ya Kariakoo kati ya Yanga na Simba, baada ya Wekundu wa Msimbazi kuandika mapema kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii kwamba hawatashiriki mechi hiyo.
Wakati sakata la Simba likizidi kuendelea ikiwa ni siku kadhaa baada ya mechi hiyo kuota mbawa na huku ikiwa haijulikani ni uamuzi gani utachukuliwa, juzi liliibuka jingine la mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly, kugomea mchezo wao wa dabi ya Cairo dhidi ya Zamalek sababu kubwa ikiwa ni kutokuwapo kwa waamuzi wa kigeni kutoka nje ya nchi hiyo. Kutokana na kushindwa kutokea uwanjani, Zamelek ilipewa pointi tatu za mezani na mabao matatu.
Hata hivyo, hii sio mara ya kwanza kwa jambo hili kutokea, hapa tumekuletea mechi nne za dabi ambazo ziliahirishwa baada ya timu moja kugomea mchezo.

BOCA JUNIOS v RIVER PLATE
Hii ilikuwa mwaka 2018 katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Amerika ya Kusini iliyozikutanisha Boca Juniors na River Plate ambazo zote zinatokea Buenos Aires, Argentina.
Timu hizi ambazo zimekuwa na ushindani wa muda mrefu, mara nyingi mechi zao zimekuwa zikigubikwa na matukio mengi ya vurugu kutokana na ushindani wao.
Mchezo wa mkondo wa kwanza wa fainali hii ulipigwa Novemba 18 mwaka huo na ukamalizika kwa sare ya mabao 2-2 na mchezo wa marudiano ukapangwa kupigwa Novemba 24.
Hata hivyo, mchezo huo haukufanyika kwa sababu ya vurugu zilizozuka nje ya uwanja zilizosababisha basi la wachezaji wa Boca kushambuliwa na baadhi yao kuumizwa na mwishowe, Boca ikaondoka kwenye eneo la uwanja.
Kutokana na hali hiyo, shirikisho la soka Amerika ya Kusini likapanga tarehe nyingine ya mchezo wa marudiano na kuamua mechi hiyo itapigwa nje ya Argentina.

Boca ilipinga suala hilo na kusisitiza kwamba hawatacheza mechi hiyo, wakaenda mbali zaidi wakifunguka kwamba River Plate haikutakiwa kushiriki kabisa mechi hiyo kutokana na vitendo vyao, hivyo wao wapewe ushindi wa mezani na ikiwa hawatasikilizwa watapeleka kesi hiyo katika mahakama ya usuluhishi wa masuala ya michezo (CAS).
Hata hivyo, CONNMEBOL ilitupilia mbali shauri hilo na baada ya hapo, Boca iliwasilisha kesi kwenda CAS ambako pia waligonga mwamba.
Mwisho mechi hiyo ikaenda kupigwa katika dimba la Santiago Bernabeu ambako ilishinda mabao 3-1 ikiwa ni jumla ya mabao 5-2 na kutawazwa kuwa mabingwa wa michuano hiyo.

ZAMALEK v AL AHLY
Mwaka 2020, Zamalek ilikumbana na adhabu baada ya kushindwa kutokea uwanjani kwa ajili ya mchezo wao wa dabi dhidi ya Ahly.
Inaelezwa moja ya sababu zilizochangia hilo ilikuwa ni kufungiwa kwa baadhi ya wachezaji muhimu wa Zamalek baada ya vurugu zilizotokea katika mchezo wa fainali ya Egyptian Super Cup wiki moja kabla ambapo Zamalek ilishinda kwa penalti.
Moja kati ya sababu ambazo Zamalek ilizotoa baada ya kushindwa kufika uwanjani ilisema walichelewa kutokana na foleni lakini chama cha soka cha Misri kilisema hakukuwa na kikwazo chochote.
Rais wa Zamalek, Mortada Mansour ambaye alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliopigwa faini katika mchezo wa Super Cup alisema hawatapeleka timu kucheza mechi hiyo kwa sababu wachezaji wake walikuwa na hofu juu ya usawa wa uamuzi katika mechi hiyo.
Hata hivyo, alibadili maoni yake na kuchagua kutuma timu ya vijana badala yake, lakini basi la timu halikuwasili uwanjani hadi saa moja baada ya muda uliopangwa wa kuanza mchezo, na kwa sababu hiyo mchezo ulimalizwa na Ahly kupata ushindi wa mabao mawili na pointi tatu, kisha Zamalek ikapokwa alama tatu na wakatakiwa kulipa faini.

ZAMALEK v AL AHLY
Katika mchezo wa dabi Juni, 18 mwaka jana, Zamalek iligoma kwenda Cairo Stadium kuvaana na Al Ahly wakitaja uamuzi usio sahihi kutoka kwa waamuzi ndio sababu kubwa.
Katika taarifa yake ya kuelezea nia ya kutoshiriki mchezo huo, Zamalek ilieleza: “Timu yetu haitaweza kucheza mchezo wa kesho wa ligi kutokana na mazingira yanayoashiria kukosekana kwa mchezo wa haki unaozingatia sheria na kanuni za soka. Tunaahidi timu itarejea kwenye mashindano siku za usoni, na tunathamini juhudi zote za vyama vyote vinavyounga mkono soka nchini Misri. Kwa kweli hatukutamani kukosekana uwanjani, lakini tulibakiwa na uamuzi huo tu.” Taarifa hiyo ilitolewa baada ya mkutano kati ya Mwenyekiti wa Zamalek, Hussein Labib, Waziri wa Michezo, Ashraf Sobhy na kiongozi wa chombo kinachosimamia ligi ya nchi huyo, Ahmed Diab katika juhudi za kuzuia kugoma kwao lakini haikufaulu.
Mivutano kati ya Zamalek, Chama cha soka, pamoja na bodi ya ligi ilijitokeza baada ya timu hiyo kufungwa mabao 2-1 na Masry katika mechi ya ligi ambayo ilishuhudiwa uamuzi tata kutoka kwa mwamuzi kuhusu penati ya Ahmed ‘Zizo’ Sayed. Kwa sababu hii, Ahly ilipewa pointi tatu na mabao mawili, kisha Zamalek ikakatwa pointi tatu pia.
Juzi timu hizo zilikuwa zikutane tena katika Ligi Kuu, lakini Al Ahly iligoma kwenda uwanjani kwa madai ya kutaka waamuzi wa kuchezesha mechi hiyo watoke nje ya nchi, jambo lililokataliwa na FA na Zamalek kupewa ushindi wa mabao matatu na pointi tatu baada ya kuibuka uwanjani na kukaguliwa freshi tu.