Karia atuma salamu za pole Dodoma Jiji

Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma salamu za pole kwa klabu ya Dodoma Jiji kufuatia ajali iliyotokea eneo la Nangurukuru mkoani Lindi.

Hayo yamebainishwa leo Jumatatu Februari 10, 2025 katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari na Mawasiliano, TFF, Clifford Mario Ndimbo.

 “Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ametuma salamu za pole kwa timu ya Dodoma Jiji kufuatia ajali ya gari iliyotokea eneo la Nangurukuru, Lindi,” imeandika taarifa na kuongeza.

“Ametoa pole kwa timu ya Dodoma Jiji kwa ajali hiyo na kuwatakia heri majeruhi wapone haraka na kurudi katika majukumu yao.”

Dodoma Jiji wamepata ajali hiyo leo asubuhi wakitoka kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo uliochezwa jana Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Awali Katibu Mkuu wa Dodoma Jiji, Fortunatus Johnson akithibitisha tukio hilo alieleza kuwa wachezaji kadhaa wamejeruhiwa kwa kukatwa na vioo vya gari baada ya kupata ajali.

“Jumla walikuwamo 37, wachezaji 25, ‘staff’15 na dereva mmoja, tayari wamepelekwa hospitali ya Nangurukuru kwa uchunguzi wa awali, hatujajua ni nani kaumia lakini ajali ni kubwa kwa kuwa walitumbukia mtoni na lile eneo ni porini”

Amesema baada ya ajali hiyo waliwasiliana na serikali ya mkoa wa Lindi ambapo walitoa msaada wa Ambulance tatu na kuwachukua majeruhi hao.