
Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia ni miongoni mwa wagombea tisa waliopita kwenye mchujo wa kuwania nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika uchaguzi utakaofanyika Machi.
Katika orodha iliyotolewa na CAF jana, Karia ni mgombea pekee wa nafasi hiyo kutoka kanda ya baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
Wagombea wengine na nchi wanazotoka ni Mustapha Raji (Liberia), Elvis Chetty (Shelisheli), Sadi Walid (Algeria), Sobha Mohamad (Mauritius), Kurt Okraku (Ghana), Feizal Sidat (Msumbiji), Alfred Randriamanampisoa (Madagascar) na Bestine Kazadi wa DR Congo.
Katika mchujo huo wa wagombea, jina moja tu ndilo limepitishwa kuwania nafasi ya Urais wa CAF ambalo ni Rais wa sasa wa shirikisho hilo, Patrice Motsepe.
Ushindani mkubwa unaonekana kuwepo katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za ujumbe wa baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ambacho kinahusisha vigogo 11 wa CAF wanaowania nafasi sita.
Washindani hao ni Djibrilla Hamidou (Niger), Isha Johansen (Sierra Leone), Lydia Nsekera (Burundi), Mathurin De Chacus (Benin), Souleiman Waberi (Djibouti), Amaju Pinnick (Nigeria), Faouzi Lekjaa (Morocco), Hany Abou Rida (Misri), Ahmed Yahya (Mauritania), Augustin Senghor (Senegal), Andrew Kamanga (Zambia), Kanizat Ibrahim (Comoro) na Yacine Diallo (Ivory Coast).