Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) na baraza la soka Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, Wallace Karia amechaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka (CAF).
Karia atakayeitumikia nafasi hiyo hadi mwaka 2029, amechaguliwa kama mwakilishi wa CECAFA na hakuwa na mpinzani kufuatia aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo, Souleiman Waberi kutoka Djibout kugombea nafasi nyingine ya uwakilishi wa CAF huko FIFA.
Waberi ambaye pia alikuwa Makamu wa Tatu wa Rais wa CAF, alisema wakati anatangaza nia ya kugombea mjumbe wa FIFA kwamba ana baraka zote za CECAFA.
Kwa kugombea kwake ujumbe wa FIFA, Waberi akawa amepoteza nafasi ya Makamu wa Rais wa CAF na kuna asilimia kubwa huu ulikuwa mpango wa CECAFA kumpa nafasi hii Karia.
Kwa kawaida, Rais wa CAF ana makamu watano; mmoja kutoka kila kanda ya kisoka ya Afrika, yaani CECAFA (Mashariki na Kati), COSAFA
(Kusini), WAFU A (Maghariki A), WAFU B (Magharibi B), UNAF
(Kaskazini).
Baada ya uchaguzi, kamati mpya ya utendaji hukutana kufanya uchaguzi
wa ndani kwa ajlli ya kuunda safu mpya ya uongozi.
Rais mpya ambaye ndiyo huongoza mkutano huo, hupendekeza jina la
mjumbe mmoja (katika waliochaguliwa) kutoka kila kanda ili kuwa makamu wake.
Halafu watu hao watapitishwa na mkutano huo na kuwa makamu rasmi wa Rais wa CAF, kuanzia makamu wa kwanza hadi wa tano.
Katika safu iliyopita, hakuna hata makamu mmoja wa rais aliyerudi kwenye uchaguzi huu.
Makamu wa kwanza, Augustin Senghor kutoka Senegal, alishindwa kwenye uchaguzi huu na akajiuzulu nafasi yake, japo ataendelea kuwa mjumbe hadi 2027.
Makamu wa pili, Ahmed Yahya kutoka Mauritania, hakugombea tena nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji bali uwakilishi wa CAF huko FIFA.
Na hivi ndivyo alivyofanya makamu wa tatu, Souleiman Waberi kutoka
Djibout, na makamu wa tano, Kanizat Ibrahim kutoka Comoro.
Makamu wa nne, Seidou Mbombo Njoya, kutoka Cameroon, ameshindwa kwenye uchaguzi huu aliosimama na Samuel Eto’o.
Mwaka 2019, Eto’o alimshinda Seidou Mbombo Njoya kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Cameroon, na sasa amemshinda kuwania ujumbe wa kamati ya utendaji ya CAF, japo vita haikuwa rahisi, Eto’o alifanyiwa mizengwe mingi ikiwemo jina lake kukatwa hadi alipofungua kesi CAS, akashinda na jina lake kurudishwa.
Hii ina maana kwamba Patrice Motsepe, Rais wa CAF aliyechaguliwa tena, atalazimika kupendekeza upya majina yote matano ya makamu wake.
Hapo ndipo nafasi ya Karia kupekendekezwa inapojitokeza. Hata hivyo,
kuna upinzani kidogo kwani Karia siyo mjumbe pekee kutoka CECAFA.
Kuna wengine wawili ambao labda Motsepe anaweza kuwafikiria juu ya
Karia, wajumbe hao ni Dkt Mutasim Gafar Sirelkhatim wa Sudan na Isayas Jira Bosho wa Ethiopia.

DK MUTASIR GAFAR SIRELKHATIM
Ni Rais wa muda mrefu wa chama cha soka cha Sudan, aliingia CAF mwaka 2023, akimshinda Moses Magogo wa Uganda ambaye alimshinda Leodger Tenga wa Tanzania mwaka 2017.
Mutasim Gafar Sirelkhatim alikuwa Rais wa CECAFA kabla ya kumpisha Wallace Karia mwaka 2019, Karia alipita bila kupingwa baada ya Mutasim Gafar Sirelkhatim kutogombea.

ISAYAS JIRA BOSHO
Ni Rais wa chama cha soka cha Ethiopia na makamu wa kwanza wa Rais wa CECAFA, Wallace Karia. Waliingia wote CECAFA mwaka 2019 kupitia uchaguzi uliofanyika pale Silversprings Hotel, Kampala Uganda.
Isayas Jira Bosho ameingia CAF safari hii kama mjumbe kupitia ‘viti maalumu’.

KARIA KUULA?
Kuna uwezekano mkubwa sana kwa Motsepe kumteua Karia kama makamu wake kutoka CECAFA badala ya hao wengine kwa sababu kuu mbili.
I. Siasa za mpira
Karia ni Rais wa CECAFA, kanda muhimu sana kimkakati kwa CAF kutokana na idadi ya wanachama wake. Kuelekea uchaguzi huu, CECAFA ilikubaliana na COSAFA kuungana mkono kwenye uchaguzi kwa kupigiana kura kwa wagombea wao.
Makubaliano hayo yalihusisha mabaraza haya kuwa na mgombea mmoja mmoja tu, kwa CECAFA akawa Karia na COSAFA akawa Rais wa chama cha soka cha Zambia, Andrew Kamanga, aliyegombea uwakilishi wa CAF huko FIFA japo ameshindwa.
Lakini hata hivyo, ushirikiano huu wa CECAFA na COSAFA anakotoka
Motsepe ni muhimu sana kuendelea ili kutuliza hali ya hewa na kuufanya utawala wa Motsepe kupata uungwaji mkono mkubwa kwenye vikao vya ndani.
Kuwa na makamu wa rais ambaye pia ni rais wa kanda muhimu kimkakati, ni jambo la afya kisiasa hasa unapotaka kuiweka mfukoni kanda hiyo.
2. Utiifu wa Karia
Wallace Karia mtiifu sana kwa Motsepe kiasi kwamba katika lugha ya mtaani tungemuita chawa wa Motsepe.
Utiifu wake kwa Motsepe umemfanya akubalike sana na ndiyo maana CAF ya Motsepe imeleta mambo mengi sana Tanzania.
Uzinduzi wa African Football League, Fainali za CHAN 2025 na AFCON 2027 na hata rais wa chama cha vilabu Afrika.
Watu wengi hawajui ilikuwaje Rais wa Yanga akawa Rais wa chama cha
vilabu, ACA. Ni kwamba wazo la kuanzisha chama cha vilabu Afrika
lilikuwa la Motsepe mwenyewe na alimtaka Moise Katumbi wa TP Mazembe awe rais.
Lakini Katumbi akakataa kwa sababu anataka kuwekeza muda na nguvu zake nyingi kwenye siasa nchini kwake DR Congo kutimiza ndoto yake ya kuwa rais.
Motsepe akaihamishia nafasi hiyo Tanzania, na mtu wa kwanza kumtaka alikuwa Mohamed Dewji (Mo Dewji), kama Rais wa Simba, lakini Mo akakataa akisema hana muda wa kutosha kuifanya kazi hiyo, akampendekeza Barbara Gonzalez, aliyewahi kuwa Mtendaji Mkuu wa Simba.
Lakini Motsepe akamkataa Barbara kwa sababu nafasi hii ilikuwa inamtaka Mwenyekiti au rais wa klabu.
Ndipo Karia mwenyewe akampendekeza Hersi Said na kumpamba sana kwa Motsepe kwamba huyu ni kijana msomi aliyeweza kuiongoza klabu kubwa kama Yanga na kuipatia mafanikio.
Motsepe akamkubali Hersi kwa imani yake kwa Karia na kulipeleka jina moja kwa moja kwenye mkutano wa kwanza wa ACA kumhalalisha tu kama taratibu zinavyotaka.
Lakini kila kitu kilishaamuliwa kwenye ‘kikao’ cha Karia na Motsepe.
Hili hata Hersi mwenyewe analijua kwa sababu aliitwa mapema na kuambiwa kuhusu mpango wa kumfanya kuwa mwenyekiti wa kwanza wa ACA.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) na baraza la soka Afrika Mashariki na Kati, CECAFA, Wallace Karia.
KARIA KATIKA NJIA YA MAGWIJI
Kwa kuingia CAF kama mjumbe wa kamati ya utendaji, Wallace Karia anakuwa Mtanzania wa tatu baada ya Said El Maamry (marehemu) na Leodeger Tenga.

El Maamry ambaye alikuwa mwenyekiti wa chama cha soka Tanzania, FAT, kuanzia 1973 hadi 1986, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF kwa vipindi vitatu kuanzia mwaka 1980 hadi 1992.
Alitoka CAF mwaka 1992, baada ya mwenyekiti wa FAT, Muhidin Ndolanga (marehemu) kuliondoa jina la EL Maamry na kulipeleka lake kwenye uchaguzi.
Kwa kanuni za CAF ni kwamba mgombea yoyote wa nafasi hii ni lazima jina lake liungwe mkono na chama cha nchi yake, basi Ndolanga akajiunga mkono yeye mwenyewe na kuliacha jina la El Maamry. Bahati mbaya akashindwa.
Mwaka 1998, CAF ikampa El Maamry ujumbe wa heshima wa kudumu kama katibu yao ilivyokuwa ikiagiza kwamba mjumbe aliyedumu kwa vipindi vitatu au zaidi atapewa heshima hiyo.
El Maamry aliendelea kuwa mjumbe wa heshima hadi alipofariki 2013.

Mwenyekiti wa mwisho wa FAT na Rais wa Kwanza wa TFF. Aliingia madarakani mwaka 2004 kurithi kiti cha Ndolanga na akakaa hadi 2013 alipong’atuka.
Tenga ambaye ni mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania katika kikosi kilichofuzu AFCON 1980, na katibu mkuu wa muda wa FAT kuanzia 1986 hadi 1989, aliingia CAF mwaka 2011 na kuhudumu kama mjumbe hadi 2017, alipoangushwa na Dk Mutasim Gafar Sirelkhatim wa Sudan.
Msudan huyu pia alimuangusha Tenga kama Rais wa CECAFA mwaka huo, kiti alichokikalia tangu 2007.
Kwa hiyo Karia ni kama amekuja kumfuta machozi Tenga kwa ubabe aliofanyiwa na Mutasim Gafar Sirelkhatim.
Kwanza kwa kuchukua kiti cha uenyekiti wa CECAFA na itakuwa bora zaidi kama atampiku kwenye umakamu wa Rais wa CAF.