
Dar es Salaam. Mfanyakazi wa duka lililopo Mtaa wa Manyema, Yohana Maziku (20), mkazi wa Mbagala, amesimulia jinsi karatasi ya oda ya mteja ya manunuzi ilivyomwepusha kwenye ajali ya kuanguka kwa jengo ghorofa.
Tukio hilo lilitokea saa 3 asubuhi ya Jumamosi Novemba 16, 2024 na mpaka sasa vifo 16 vimeripotiwa pamoja na majeruhi zaidi ya 80.
Kwa mujibu wa Yohana, siku hiyo walipigiwa simu na mteja wao akiwataka kufika dukani mapema kwa ajili ya kumfungia mzigo wenye thamani ya Sh4 milioni, akikusudia kuusafirisha kwenda Mbeya.
Amesema duka lao liko mtaa wa Manyema na stoo ilikuwa kwenye ghorofa lililoporomoka mtaa wa Mchikichi.
“Kutokana na ufinyu wa duka letu, tulihifadhi baadhi ya bidhaa katika stoo iliyokuwa kwenye ghorofa la pili la jengo hilo lililoanguka,” amesema Yohana.
Baada ya kumaliza kuandaa oda ya mteja wake, Yohana alichukua karatasi kwenda stoo kuchukua mzigo. Alipofika, aligundua alikuwa amebeba karatasi tofauti, hivyo alilazimika kurudi dukani kuchukua ile oda.
“Nilipokuwa narudi stoo, nilipofika kona ya Mtaa wa Mchikichi, ghafla niliona vumbi zito likipaa. Nilipoangalia vizuri, nikaona jengo limeanguka. Nilichofanya ni kukimbia haraka hadi dukani kumwambia bosi wangu,” amesema Yohana.
Amesimulia jinsi watu walivyokuwa wakipiga kelele kuomba msaada, wengine wakikimbia huku vumbi likiwa zito kiasi cha kutojua nani ni nani.
Baada ya muda, walirudi eneo la tukio kushuhudia uokoaji. Hata hivyo, hofu ya usalama wao na maonyo ya polisi yaliwazuia kusogea karibu na stoo yao, ambayo haikuwa sehemu ya mbele ya jengo.
“Watu waliohifadhi mizigo karibu na sehemu ya mbele walijaribu kutoa bidhaa zao, lakini polisi walifika na kutuzuia. Walitwambia tusikaribie kwa kuwa jengo lingeweza kuanguka zaidi,” amesema Yohana.
Ameongeza tukio hilo limewaacha na hofu kubwa, hadi kufikia hatua ya kulala kwenye korido za maduka jirani bila kurejea nyumbani, wakisubiri hatima ya mizigo yao.