Kapteni Traore atoa msimamo wanajeshi 21 waliojaribu kupindua Serikali

Ouagadougou. Rais wa mpito wa Burkina Faso, Kapteni, Ibrahim Traoré, amewasamehe wanajeshi 21 waliokutwa na hatia ya kujaribu kupindua Serikali ya nchi hiyo karibu muongo mmoja uliopita.

Taarifa ya kusamehewa kwa wanajeshi hao imetolewa jana Jumatatu Machi 31, 2025na kuchapishwa  na vyombo vya habari vya ndani siku ya Jumatatu.

Inaripotiwa kuwa Traoré alitangaza msamaha Desemba mwaka jana kwa watu kadhaa waliokuwa wamehukumiwa kwa kupanga njama ya kupindua Serikali ya mpito mwaka 2015, baada ya kujiuzulu kwa lazima kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Blaise Compaoré.

Compaoré alitwaa madaraka kupitia mapinduzi ya mwaka 1987 baada ya kumuua Rais wa wakati huo na Mwanaharakati wa Uafrika, Thomas Sankara.

“Kwa watu wafuatao, ambao wamehukumiwa au kushtakiwa mahakamani kwa matendo waliyofanya Septemba 15 na 16, 2015, wanapewa msamaha,” Traoré alitangaza katika amri hiyo, iliyotiwa saini Machi 24, akiwataja wanajeshi 21.

Maofisa hao, wakiwemo makamanda wawili wa zamani wa kikosi cha Ulinzi wa Rais, walihukumiwa na mahakama ya kijeshi mjini Ouagadougou mwaka 2019 kwa makosa ya kuhatarisha usalama wa taifa, mauaji, na usaliti.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari  la AFP, Mkuu wa zamani wa Majeshi wa Compaoré, Gilbert Diendéré, na Mkuu wa zamani wa Diplomasia, Djibril Bassolé, ambao ni majenerali wawili waliohukumiwa kifungo cha miaka 20 na 10 mtawalia kwa madai ya kuongoza jaribio hilo la mapinduzi, hawajajumuishwa katika msamaha huo.

Wanajeshi waliosamehewa watarejea katika jeshi la taifa kupambana na ugaidi nchini humo.

Traoré aliahidi mwaka jana kurejesha maeneo yote ya nchi yaliyo chini ya udhibiti wake kutoka kwenye mikono na udhibiti wa magaidi kufikia mwisho wa mwaka 2025.

Koloni hilo la zamani la Ufaransa limekuwa likipambana na makundi ya Kijihadi tangu 2015, yakiwemo yale yenye mafungamano na Al-Qaeda.

Traoré alitwaa madaraka mwaka 2022 baada ya mapinduzi mawili ya kijeshi.

Mapinduzi ya kwanza yalifanyika Januari mwaka huo, ambapo jeshi lilimuondoa madarakani Rais wa zamani, Roch Kaboré, likimtuhumu kushindwa kudhibiti uasi wa wanamgambo wa Kiislamu.

Baadaye, Traoré aliongoza mapinduzi ya pili Septemba, yaliyomuondoa kiongozi wa mpito aliyekuwa madarakani, Luteni Kanali, Paul-Henri Sandaogo Damiba.

Agosti mwaka jana, nchi hiyo isiyo na pwani ilikumbwa na moja ya mashambulizi mabaya zaidi tangu uasi huo uanze kuenea kutoka Mali zaidi ya muongo mmoja uliopita.

Takriban watu 200 waliuawa na wengine 169 walijeruhiwa na wanamgambo wa Kiislamu walipofyatua risasi kwa raia waliokuwa wakichimba mitaro ya kujihami katika mji wa Barsalogho, kaskazini mwa nchi hiyo.

Burkina Faso na majirani zake, Mali na Niger, ambazo pia ziko chini ya utawala wa kijeshi, zilikata uhusiano wa ulinzi na mkoloni wao wa zamani, Ufaransa, wakidai kuingiliwa na kushindwa kwa vikosi vya Kifaransa kutuliza hali ya usalama.

Nchi hizo tatu zimeunda kundi jipya Muungano wa Mataifa ya Sahel na zimeanza kushirikiana na Russia katika masuala ya usalama, ambapo Moscow imekubali kuwasaidia katika juhudi za kukabiliana na ugaidi.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *