Kapombe na siku 811 ngumu Stars

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la Taifa Stars hapana shaka limerejesha furaha kwa beki wa kulia wa Simba, Shomary Kapombe baada ya mchezaji huyo kupita siku 811 za kusubiri wito wa uteuzi.

Kutoteuliwa kwa Kapombe katika kipindi hicho cha wiki 115 na siku sita, kumemfanya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 32 kuzikosa fainali za mataifa ya Afrika (Afcon), zilizofanyika mwanzoni mwa mwaka huu huko Ivory Coast ambazo Taifa Stars ilishiriki.

Kapombe pia alikosa mechi 18 za mashindano tofauti rasmi ambapo mechi tatu ni za Afcon, mechi tatu za mashindano ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia na mechi nane za mashindano ya kuwania kufuzu Afcon.

Licha ya kutopata nafasi kwenye kikosi cha Taifa Stars, Kapombe katika kipindi chote hicho aliendelea kuwa mchezaji tegemeo wa Simba na kusaidia katika mafanikio ya kutinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja na kumaliza katika nafsi ya pili kwenye msimamo wa ligi mara mbili huku ikifanikiwa kutwaa taji la Kombe la Muungano.

Katika kipindi hicho cha siku 811 ambacho Kapombe hakubahatika kuteuliwa katika kikosi cha Taifa Stars, timu hiyo imenolewa na makocha wanne tofauti ambao ni Honour Janza, Adel Amrouche , Hemed Morocco na Bakari Shime lakini ni Morocco ambaye amemrudisha kikosini kwa ajili ya kumtumia katika mechi mbili za kuwania kufuzu Afcon 2025 dhidi ya Ethiopia, Novemba 16, ikiwa ugenini na siku tatu baadaye itakuwa nyumbani katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kikosi cha Taifa Stars kimeteuliwa mara 13 tofauti katika kipindi hicho ambacho Kapombe amekosekana ambapo ilikuwa ni katika mashindano ya Afcon, kuwania kufuzu Afcon, kuwania kufuzu Kombe la Dunia, kuwania kufuzu Chan na pia mechi za kirafiki.

Akizungumzia uteuzi wa Kapombe, kocha wa Taifa Stars, Hemed Morocco alisema kuwa amejumuishwa kikosini kwa vile ameonyesha kiwango bora ndani ya klabu yake.

“Kapombe na wengine wamestahili pia kuwemo kwa sababu hii ni timu ya taifa na yeyote anayeonyesha uwezo mkubwa anastahili kuwepo. Matumaini yetu ni kuona tunafuzu Afcon mwakani mwakani na ndio maana tumeita kikosi bora cha kutimiza malengo hayo,” alisema Morocco.    

Baada ya kuiongoza Taifa Stars katika mechi mbili za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan), kipa Aishi Manula ameendelea kujumuishwa katika kikosi cha timu hiyo huku kipa aliyedaka mechi nne zilizopita za kuwania kufuzu Afcon, Ally Salim hajawekwa kundini.

Kocha Morocco alisema kuwa kuitwa kwa Manula kumetokana na kiwango alichoonyesha katika mechi za kuwania kufuzu fainali za Chan.

“Ni kweli Manula amekuwa hana michezo mingi ya ushindani, lakini baada ya kumuona katika mechi hizi mbili na Sudan tumeona anaweza pia kutuongezea kitu cha ziada kwa wote waliopo,” amesema kocha huyo.

Kuna urejeo wa nyota wa Al-Talaba ya Iraq, ASaimon Msuva ambaye hakucheza mechi nne zilizopita za kuwania kufuzu Afcon dhidi ya DR Congo, Guinea na Ethiopia.

Kiungo Novatus Dismas anayeitumikia Goztepe ya Uturuki, naye amerudi kikosini baada ya kukosekana dhidi ya DR Congo lakini beki aliyedumu kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Taifa Stars, Novatus Miroshi naye amejumuishwa katika kikosi cha timu hiyo.

Kuna ingizo la wachezaji wanne ambao walikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza mechi za kuwania kufuzu Chan dhidi ya Sudan ambao ni Ibrahim Ame, Manula, David Bryson na Abdulkarim Kiswanya.

Kikosi hicho cha Taifa Stars kilichotangazwa jana kinaundwa na wachezaji 26 na kitaingia kambini leo jijini Dar es Salaam.

Wachezaji walioitwa ni makipa, Aishi Manula (Simba), Ziberi Foba (Azam FC) na Metacha Mnata wa Singida Black Stars huku mabeki wakiwa ni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Abdulrazack Hamza (Simba), Lusajo Mwaikenda na Pascal Msindo wa Azam FC.

Wengine ni Ibrahim Hamad ‘Bacca’, Dickson Job, (Yanga), Ibrahim Ame (Mashujaa) na David Bryson kutoka JKT Tanzania.

Viungo ni Adolf Mtasingwa, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Nassor Saadun (Azam FC), Mudathir Yahya (Yanga),  Kibu Denis (Simba), Novatus Dismas (Goztepe), Habib Khalid (Singida Black Stars) na Abdulkarim Kiswanya (Azam FC U-20).

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (PAOK), Cyprian Kachwele (Vancouver Whitecaps), Clement Mzize (Yanga), Idd Seleman ‘Nado’ (Azam FC), Ismail Mgunda (Mashujaa) na Simon Msuva (Al-Talaba).

Mchezo dhidi ya Ethiopia utachezwa Novemba 16 katika Uwanja wa Martyrs de la Pentecôte uliopo Kinshasa, DR Congo na dhidi ya Guinea utachezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Novemba 19.

Taifa Stars inashika nafasi ya tatu katika msimamo wa kundi H ikiwa na pointi nne huku kinara ikiwa ni DR Congo yenye pointi 12 na Guinea inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi sita huku Ethiopia yenye pointi moja ikishika mkia.

Timu mbili zitakazoongoza kundi hilo zitafuzu fainali za Afcon ambazo mwakani zitafanyika Morocco.