Kanuni zifuatwe kwa Simba, Yanga

Tukio la kuahirishwa kwa mechi ya watani wa jadi, Yanga dhidi ya Simba, ni pigo kubwa kwa maendeleo ya soka letu. Licha ya maendeleo makubwa yaliyopatikana katika miaka ya hivi karibuni na ligi yetu kutangazwa kuwa inashika nafasi ya nne kwa ubora lakini hili ni pigo kubwa.

Shida kubwa siyo kuahirishwa kwa mchezo, bali kutofuatwa kanuni ambazo zimewekwa ili mchezo husika uweze kuahirishwa.

Matukio kama haya yanaweza kurudisha nyuma jitihada za kuinua hadhi ya ligi yetu kwa kuwa inaonekana kuna mambo yanaweza kufanyika kienyeji kwa ajili ya maslahi ya watu wachache kwenye soka letu.

Hii siyo mara ya kwanza kwa timu za Simba na Yanga kuingia kwenye kadhia kama hii, lakini mara zote kanuni zimekuwa hazifuatwi na baadaye kila kitu kinaonekana kwenda sawa, siyo jambo zuri hata kidogo kwa soka letu.

Kwanza, uamuzi wa Simba SC kugomea mechi kwa madai ya kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho haionyeshi kama kulikuwa na athari kubwa ambayo inaweza kulazimisha mchezo huu kuahirishwa kwa kuwa kama ni maandalizi tayari Simba walishafanya na walikuwa wanakwenda kukamilisha tu, mara nyingi siyo zaidi ya saa moja.

 Soka ni mchezo wa sheria na kanuni na kama kuna mgogoro wowote, njia sahihi ni kufuata taratibu za kikanuni badala ya kuchukua maamuzi ambayo yana madhara makubwa kwa ligi, wadau na mashabiki wa mchezo huu kwa ujumla.

Pili, Bodi ya Ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), zinapaswa kubeba lawama kwa jinsi suala hili lilivyoshughulikiwa, kama mechi ilipaswa kuchezwa, ni kwanini Bodi ya Ligi ilichelewa kutoa tamko la kuiahirisha hadi saa chache kabla ya muda wa mchezo? Ucheleweshaji huu ulisababisha athari kubwa kwa mashabiki waliokwishaingia uwanjani, baadhi yao wakitoka mikoani na kuingia gharama za usafiri, chakula na malazi.

 Wafanyabiashara waliotegemea mechi hii kuuza bidhaa zao walipata hasara kubwa na hakuna ambaye anaweza kuwalipa.

Tatu, msimamo wa Yanga wa kusema haitacheza mechi hiyo tena katika tarehe nyingine unaongeza ugumu wa hali hii. Endapo klabu moja inaweza kugomea mechi na nyingine ikakataa kucheza tarehe mpya, inamaanisha tunaendesha soka letu kwa matakwa ya klabu badala ya kufuata kanuni. Ligi yoyote duniani inapaswa kuwa na mifumo thabiti ya kushughulikia mambo kama haya bila kuathiri kanuni na taratibu za mashindano.

Aidha, tukio hili linaathiri kwa kiasi kikubwa taswira ya soka la Tanzania kimataifa, ligi yetu inashika nafasi ya nne barani Afrika kwa mujibu wa IFHHS, lakini matukio kama haya yanaweza kufanya wadhamini na wadau wa kimataifa kupoteza imani na ubora wa ligi yetu.

Suluhisho ni nini? Ni wakati sasa kwa TFF na Bodi ya Ligi kuwa na msimamo thabiti na kuhakikisha kanuni zinaheshimiwa na kutekelezwa kwa haki bila upendeleo wa timu hizi kubwa za Simba na Yanga.

Klabu zisiruhusiwe kugomea mechi kiholela na migogoro yoyote inayojitokeza inapaswa kushughulikiwa kwa haraka ili kuepusha madhara makubwa kwa ligi yetu, kwa kuwa huko mbele kunaweza kutokea jambo lingine kubwa zaidi.

Viongozi wa soka wanapaswa kuonyesha kuwa wana mamlaka ya kusimamia mchezo huu kwa weledi na si kwa upendeleo au kulinda maslahi ya Simba na Yanga tu.

Tunaamini kama hali hii ingekuwa imetokea kwa timu nyingine ndogo basi adhabu ingekuwa kubwa kwao, ni vyema kama kwa wengine inafanyika hivyo basi hali hiyo iwe pia kwa timu za Simba na Yanga bila kujali ukubwa wao.