Wawakilishi wa Kanisa Katoliki (RC) lenye ushawishi mkubwa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamekutana na Kiongozi Mkuu wa Muungano wa Waasi (AFC/M23), Corneille Nangaa kujadili namna ya kurejesha amani Mashariki mwa nchi hiyo.
Kikao kilichowakutanisha viongozi hao wa dini na uongozi wa waasi ulifanyika jana Jumatano Februari 12, 2025, zikiwa zimepita wiki tatu tangu M23 watangaze kuyatwaa maeneo ya Jimbo la Kivu Kaskazini ikiwemo Mji Mkuu wa jimbo hilo, Kivu.
Shirika la Habari la Reuters limeripoti mkutano huo ulifanyika mjini Goma huku kiongozi wa waasi, Corneille Nangaa, akijaribu kujitambulisha kama msemaji wa wanasiasa na makundi ya waasi yanayompinga Rais wa DRC, Félix Tshisekedi.
Kundi la Nangaa, linaloitwa Alliance Fleuve Congo (AFC) na linaloiona M23 kama kitengo chake cha kijeshi, limekuwa likiudhibiti Mji wa Goma, ambao ni Mji Mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, tangu mwishoni mwa Januari.
Jumanne wiki hii, lilitishia kuendeleza mashambulizi kuelekea Bukavu ambao ni Mji Mkuu wa Kivu Kusini.

Vyanzo viwili vya Umoja wa Mataifa (UN) na gavana wa jimbo la Kivu Kusini walisema jans Jumatano kuwa M23 sasa inadhibiti mji wa Ihusi uliopo magharibi mwa Ziwa Kivu, kati ya Mji wa Goma na Bukavu.
“Tumearifiwa Ihusi imechukuliwa na maadui,” amesema Gavana wa Kivu Kusini, Jean-Jacques Purusi Sadiki, akiongeza kuwa vikosi vya Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC), vilikuwa vikiendeleza mashambulizi ya kujihami dhidi ya waasi hao.
Miji ya Bukavu na Kavumu, ni miji ya kimkakati na iliyo umbali wa takriban Kilomita 35, Kaskazini mwa DRC. Mji wa Kavumu ndipo ulipo uwanja wa ndege ambao unadaiwa kudhibitiwa na Jeshi la FARDC, linalosaidiwa na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali pamoja na vikosi vya nchi jirani ya Burundi.
Ofisa wa Kanisa Katoliki, ambaye hakutaka kutajwa jina lake, aliieleza Reuters mwishoni mwa wiki mkutano na Nangaa, ulilenga kushinikiza kupatikana kwa muundo wa mazungumzo unaokubalika kati ya waasi na Serikali ya Rais Tshisekedi.
Baada ya mkutano huo, Donatien Nshole, ambaye ni Katibu Mkuu wa Mkutano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki alisema maofisa wa kanisa walihimiza kufunguliwa upya kwa uwanja wa ndege wa Goma na bandari yake pamoja na kutaka usitishaji wa mapigano.
Ofisi ya Tshisekedi ilichapisha taarifa kwenye mtandao wa X (zamani Twitter), Jumatano kuwa Rais alikutana na viongozi mbalimbali wa kidini na yuko tayari kwa juhudi za upatanisho za Kanisa Katoliki, mradi tu ziwe za ujumuishi.
Vita ya Kikanda
Kujitanua kwa kundi la M23 na uwezekano wa mapigano makali mjini Bukavu yameongeza hofu ya kuzuka kwa vita vikubwa zaidi vya kikanda ambapo majeshi ya mataifa jirani yanaweza kujikuta yakipambana kama ilivyoshuhudiwa katika vita vya awali kati ya mwaka 1996 na 2003.
DRC, UN na mataifa kadhaa ya Magharibi wameituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi hao kwa kuwatuma maelfu ya wanajeshi wake pamoja na kuwapa silaha nchini DRC.

Hata hivyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame kupitia mahojiano yake na CNN ilikanusha vikali kuwaunga mkono M23 huku akisema hana taarifa ya uwepo wa askari wa Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), ndani ya mipaka ya DRC.
Pia, Kagame alisema ikitokea kuna wanajeshi wake wamevuka mpaka hadi ng’ambo ya DRC, Operesheni hiyo inakuwa ya hatua za kujilinda.
Katika hatua nyingine, Shirika la Ndege la Rwanda, RwandAir, limesema Jumatano kuwa limelazimika kubadilisha njia za safari zake baada ya DRC kufunga anga na kutoruhusu ndege zilizosajiliwa nchini Rwanda kupita katika anga hilo.
Mapigano yaliyoshika kasi tena mashariki mwa DRC tangu, 2022 yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 3,000 na kusababisha zaidi ya milioni moja kuyakimbia makazi yao.