Kanga kutumika kuhamasisha AFCON

Dodoma. Bunge limetangaziwa rasmi kuwa vazi la kanga litatumika kama nyenzo ya kimkakati ya uhamasishaji katika fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 zitakazofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.  

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi ameyasema hayo leo Mei 7,2025 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka 2025/26.

Profesa Kabudi ameomba Bunge kumuidhinishia Sh519.66 bilioni huku miradi ya Maendeleo ni Sh458.19 bilioni.

“Naomba kutumia fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa vazi la kanga litatumika kama nyenzo ya kimkakati ya uhamasishaji katika michuano ya AFCON 2027 itakayofanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda na litaendelea kutumika kukieneza Kiswahili duniani kote,”amesema Kabudi.

Aidha, Profesa Kabudi amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuhakikisha kunakuwa na soko la uhakika la kazi za filamu na muziki nchini.

“Moja ya hatua zilizochukuliwa ili kufikia azma hiyo Wizara inafanya jitihada za kuingia makubaliano na wamiliki wa Kampuni za Falme za Kiarabu, ambapo mazungumzo ya awali yalifanyika Novemba 15, 2024, jijini Dubai,”amesema.

Amesema pia imefanikiwa kuandaa andiko la ushirikiano baina ya Tanzania na Benki ya Dunia.

Amsema ushirikiano huo, pamoja na maeneo mengine, utaiwezesha Serikali kujenga vituo vya Sanaa na Utamaduni katika ngazi ya Mikoa kupitia Country Partnership Framework 2025 – 2029.

Amesema ujenzi wa vituo hivyo utatoa nafasi kwa wadau kuendesha shughuli za sanaa na utamaduni.

Amesema vituo hivyo vitawezesha kufunguliwa kwa ofisi za mikoa za Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA),  Baraza la Kiwahili la Taifa (BAKITA), Bodi ya Filamu, Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania.

Amesema sambamba na ujenzi wa vituo, andiko pia linalenga kuboresha mifumo ya kidijiti 65 ya utendaji kazi wa COSOTA,

Aidha, Profesa Kabudi amesema watatunisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania pamoja na kuanzisha Makao Makuu ya Sanaa kwa Walemavu hapa nchini.

Amesema katika mwaka katika mwaka wa fedha wa 2025 na 2026, mradi wa ujenzi wa Film Studio and Multipurpose Entertainment Complex wenye thamani ya Sh450 bilioni ni mmoja wa miradi itakayojengwa katika mpango wa fedha kutoka Korea Kusini.

“Mradi huu utakapokamilishwa, sio tu Tanzania itapata fursa ya kuingiza fedha za kigeni kupitia kampuni zitakazokuja kufanya shughuli za filamu na burudani hapa nchini,”amesema.

Amesema pia itaongeza thamani kwa wasanii wetu na kuonesha namna ambavyo Tanzania inaithamini Sekta ya Sanaa na burudani katika kuzalisha ajira, kuongeza kipato kwa wadau wake na kuchangia kikamilifu katika Pato la Taifa.

Aidha, amesema katika kusimamia maslahi ya wasanii, baraza limefanya vikao vya utatuzi wa migogoro ya wasanii wa muziki kupitia Dawati la Sheria, Maadili na Usuluhishi.

“Kati ya migogoro 18 iliyopokelewa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025 migogoro 15 ilitatuliwa na migororo mitatu (3) ipo kwenye hatua tofauti za utatuzi. Mwenendo unaonesha kwamba migogoro ya kimasilahi baina ya wadau wa sanaa 69 imekuwa inapungua kutokana na hatua ambazo Baraza kupitia Dawati hilo, imekuwa inachukua ikiwamo kutoa elimu na ushauri kwa wadau kuhusu masuala ya mikataba ya kazi za sanaa,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *