Harry Kane amekuwa mchezaji wa kwanza raia wa England kufunga mabao 10 katika msimu mmoja wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuiongoza Bayern Munich kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Bayer Leverkusen jana usiku.
Ni bao moja tu ambalo limemfanya Kane aweke rekodi hiyo ambalo amefunga katika dakika ya 52 akimalizia mpira wa faulo uliopigwa na Joshua Kimmich na bao la pili lilipachikwa na Alphonso Davies katika dakika ya 71 akimalizia pasi ya Kane.
Matokeo hayo yameifanya Bayern Munich kufuzu kwa ushindi wa jumla ya wa mabao 5-0 ambapo sasa itakutana na Inter Milan katika hatua ya robo fainali.

Mshtuko umekuwa katika Uwanja wa Anfield ambako wenyeji Liverpool wamejikuta wakiondoshwa katika mashindano hayo baada ya kuchapwa kwa mikwaju ya penalti 4-1 na PSG.
Katika dakika 120, PSG iliibuka na ushindi wa bao 1-0, matokeo yaliyolazimisha mshindi baina ya timu hizo kupatikana kwa mikwaju ya penalti kwani mechi ya kwanza, Liverpool ilipata ushindi wa bao 1-0 ugenini huko Ufaransa.
Kwingine, Barcelona na Inter Milan zimemalizia vyema kazi nzuri ambazo zilifanya katika mechi za kwanza ugenini kwa kupata ushindi kwenye mchi za pili nyumbani ambao umezisogeza robo fainali.

Barcelona imeibuka na ushindi wa mabao 3-1 nyumbani ambao umeifanya isonge mbele kwa jumla ya mabao 4-1 dhidi ya Benfica huku Inter Milan ikiichapa Feyenoord kwa mabao 2-1, matokeo ambayo yameipeleka robo fainali kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-1