Kamwe, Mazanzala wapelekwa kamati ya maadili TFF

 Kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania iliyoketi Dar es Salaam Jumatano, Februari 12, 2025  imetembeza rungu kwa Pamba Jiji FC huku ikimpeleka katika kamati ya maadili ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo, Februari 24, 2025 imeeleza kuwa Pamba imetozwa fain ya fedha kwa kosa la mashabiki wake kuingia uwanjani baada ya mchezo dhidi ya Azam FC uliochezwa Februari 9, 2025.

“Klabu ya Pamba Jiji ya Jijini Mwanza imeadhibiwa kwa kutozwa faini ya Sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kosa la mashabiki wake kuvamia eneo la kuchezea (kiwanja) mara baada ya mchezo tajwa hapo juu kumalizika.

 Kitendo cha mashabiki hao kuingia kiwanjani kilisababisha kuvunjika kwa mahojiano ya makocha yaliyokuwa yakifanywa na mdhamini mwenye haki ya matangazo ya runinga, Azam TV. Adhabu hii ni kwa mujibu wa kanuni ya 17:(50 & 62) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo,” ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo.

TPLB imeweka angalizo kuwa uwanja wowote unaotumika kwa mechi za Ligi Kuu utafungiwa iwapo mashabiki wataingia uwanjani.

“Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imezielekeza klabu zote, wasimamizi wa vituo na maofisa wengine wa michezo ya Ligi (wakiwemo maofisa usalama), kuhakikisha matukio ya aina hii hayatokei tena viwanjani kwa sababu yanahatarisha usalama na kuchafua hadhi ya Ligi.

 “Uwanja wowote ambao litatokea tukio la mashabiki kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) kabla, wakati au baada ya mchezo wa Ligi, utafungiwa kutumika kwa michezo ya Ligi,” imesema taarifa hiyo.

Adhabu ya Pamba imeenda sambamba na uamuzi wa kamati ya uendeshaji na usimamizi wa ligi kumpeleka ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe na mwenzake wa Kagera Sugar, Hamis Mazanzala kwa kosa la kuandika maandiko ya uchonganishi.

“Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imewapeleka kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Ofisa Habari wa klabu ya Yanga Bw. Ali Kamwe na Ofisa Habari wa klabu ya Kagera Sugar, Bw. Hamis Mazanzala kwa tuhuma za kutenda makosa ya kimaadili kupitia machapisho yao kwenye kurasa za mtandao wa kijamii wa Instagram

“Viongozi na maofisa wa klabu wanazuiliwa kwa mujibu wa kanuni kutoa maandiko au matamshi chonganishi ama yanayoweza kuchafua taswira ya Ligi na mpira wa miguu kwa ujumla.

“Bodi inawakumbusha Maofisa Habari/Wasemaji wa klabu zote kuzingatia kanuni za Ligi na za maadili wakati wote wanapotekeleza majukumu yao ili kuepuka kutoa kauli ambazo zinaweza kuzua chuki, taharuki au kuchochea,” imesema taarifa hiyo ya bodi.

Katika hatua nyingine timu za Kiluvya United na African Sports za ligi ya Championship zimepewa onyo kali.

“Klabu za Kiluvya ya mkoani Pwani na African Sports ya mkoani Tanga zimepewa Onyo kwa kosa la kuchelewa kuwasili uwanjani kinyume cha matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Championship kuhusu Taratibu za Mchezo.

 “Klabu ya Kiluvya iliwasili uwanjani saa 8:43 mchana huku klabu ya African Sports ikiwasili uwanjani saa 8:40 badala ya saa 8:30 mchana. Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 17:62 ya Championship kuhusu Taratibu za mchezo,” imefafanua TPLB.