Kamwe atozwa faini, Ahmed Ally akiponea rungu TFF

Dar es Salaam. Kamati ya maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limempa adhabu ya faini na onyo ofisa habari wa Yanga, Ally Kamwe kwa kosa la kukiuka kanuni za maadili.

Katika taarifa ya kamati hiyo iliyotolewa leo, Aprili 19, 2025, imeeleza kwamba Kamwe amekutwa na hatia hivyo kumpa adhabu hiyo.

“Ally Kamwe, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Yanga, alishtakiwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi akituhumia kwa kosa la kuchochea umma kwa ujumla kinyume na Kanuni 73(4) ya Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la Mwaka 2021.

“Baada ya kusikiliza pande zote na kupitia nyaraka na vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake, Kamati imemtia hatiani kwa kosa aliloshtakiwa nalo na kumpa adhabu ya kulipa faini ya sh. 5,000,000 (milioni tano) na onyo la kutofanya kosa la kimaadili dani ya kipindi cha miaka miwili. Adhabu hiyo inaanza tarehe 16/04/2025,” imefafanua taarifa hiyo.

Kauli ya uchochezi ambayo Kamwe anatuhumiwa kutoa ni ya kudai waamuzi wanaipendelea timu ambayo hakuitaja jina.

“Na leo sio mara ya kwanza, Huu ni muendelezo. Ni kama Mechi ya 10 Mfululizo, Kila mechi ya Kolo huwa na Mijadala redioni kuhusu Makosa ya Waamuzi yanayowanufaisha KOLO kupata Ushindi.

“Mara wapinzani wanayimwa Magoli Halali, Mara mjadala wa Kolo akifunga Magoli ya Offside na waamuzi wanayakubali. Tumesikia pia Mijadala ya Penalti nyingi za mchongo zikiwanufaisha Makolo.

“This is Is Too Much .. Na inatupa Wasiwasi kama Haya Yanayotokea, huwa yanatokea kwa Bahati mbaya kwa kichaka cha ‘Makosa ya Kibinadamu’,” ni baadhi ya nukuu ya maneno yaliyomtia hatihani Ałły Kamwe.

Kamati hiyo pia imemuachia huru Ahmed Ally kwa vile mashitaka yake hayakuweza kuthibitishwa.

Mbali na uamuzi kuhusu Kamwe na Ahmed Ally, kamati hiyo pia imetoa adhabu kwa wanafamilia wengine wa mpira wa miguu.

Ofisa habari wa Kagera Sugar, Hamisi Manzazala ametozwa faini ya Shilingi 5 milioni na onyo kwa kosa kutoa kauli za uchochezi.

Shufaa Nyamlani amefungiwa maisha kujihusisha na soka baada ya kukutwa na hatia ya kutoheshimu uamuzi wa TFF.

Salehe Mohamed amefungiwa maisha kujihusisha na soka kwa kosa la uchochezi na kutoheshimu uamuzi wa TFF.

Adhabu hizo zote zimeanza tangu Aprili 16, 2025.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *