Kampuni ya Euro Vista yaamriwa kuilipa TIB Sh9.8 bilioni

Arusha. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Dar es Salaam, imeiagiza Kampuni ya Euro Vistaa Tanzania Limited kuilipa Benki ya Maendeleo ya Tanzania (TIB) zaidi ya Sh9.8 bilioni, ikiwa ni mkopo uliopaswa kulipwa kufikia Februari 24, 2024.

Mbali na deni hilo la msingi, Mahakama imeiamuru kampuni hiyo ilipe riba ya asilimia saba kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo yote yatakapokamilika.

Amri hiyo ilitolewa na Jaji Awamu Mbagwa Aprili 14, 2025, baada ya kukubali madai ya benki hiyo katika kesi ya madai. TIB ilikuwa mdaiwa wa kwanza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali mdaiwa wa pili kwa mujibu wa sheria, kwa kuwa na maslahi katika shauri hilo.

Kampuni ya Euro Vistaa, iliyokuwa mdaiwa wa kwanza, ilishtakiwa pamoja na Gidarilal Lath na Yuvraj Pramond Lath, ambao walikuwa wadhamini wa mkopo huo uliotolewa kwa kampuni hiyo inayojihusisha na biashara jijini Dar es Salaam.

Shauri hilo liliamuliwa upande mmoja wa mdai (TIB), baada ya wadaiwa kushindwa kufika mahakamani, licha ya kuitwa kwa notisi iliyochapishwa kwenye Gazeti la Mwananchi la Agosti 27, 2024.

Pamoja na wito huo, wadaiwa hawakuwasilisha majibu ya maandishi ya utetezi wao dhidi ya madai hayo.

Hivyo, Septemba 25, 2024, Mahakama ilitoa amri ya kusikiliza kesi hiyo upande mmoja kwa mujibu wa Amri ya VIII, Kanuni ya 14 ya Kanuni za Mwenendo wa Mashauri ya Madai.

Benki ya TIB iliomba Mahakama itamke kuwa wadaiwa walikiuka masharti ya mkataba wa mkopo, na hivyo iwaamuru walipe kiasi kilichobaki cha Sh9.8 bilioni baada ya kulipa Sh600 milioni pekee.

Benki hiyo pia iliomba kulipwa riba ya asilimia 27 ya deni lililobaki kuanzia tarehe ya kushindwa kulipa hadi tarehe ya hukumu, pamoja na riba ya kiwango kinachotolewa na Mahakama kuanzia siku ya hukumu hadi malipo kamili.

Katika usikilizwaji wa shauri hilo, mdai aliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Tausi Sued. Kwa upande wa ushahidi, mdai aliwasilisha shahidi mmoja, Emanuel Bushiri, pamoja na vielelezo 15 vikiwemo mkataba wa mkopo uliosainiwa Januari 27, 2008.

Kwa mujibu wa ushahidi, kampuni hiyo iliomba mkopo wa Dola 300,000 za Marekani kwa ajili ya ununuzi wa mbegu, mbolea, pampu tatu, jenereta moja na gharama nyingine za uendeshaji. Baadaye, mkopo huo uliongezwa hadi kufikia Dola milioni 2.2.

Hata hivyo, mdaiwa alishindwa kurejesha mkopo huo ndani ya muda ulioainishwa, licha ya kupewa notisi ya siku 60.

Mali zilizowekwa rehani ziliuzwa na mapato yake yakatumika kulipa sehemu ya mkopo, na kubaki deni la Sh9.8 bilioni hadi kufikia Februari 24, 2024.

Baada ya kusikiliza ushahidi na vielelezo vya mdai, Mahakama iliridhika kuwa madai hayo yamethibitishwa kwa kiwango kinachotakiwa kisheria, na hivyo kutoa amri hiyo dhidi ya wadaiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *