Kambi ya Jabalia, “Hiroshima” ya Gaza, ambayo inafutwa na utawala ghasibu wa Israel

Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukijaribu kuwaondoa kwa nguvu wakazi wa Kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, kwa kuweka mzingiro mkali na kufanya uharibifu mkubwa wa nyumba na majengo ya eneo hilo, kuzuia kuingia na kutoka isipokuwa kupitia vituo vya ukaguzi ambavyo umeviweka kwa ajili yay kufanya upekuzi kwa wakimbizi wanaoeleka kusini mwa Gaza.

Klipu za video na picha za kipindi cha mwaka mzima wa vita zimesajili uharibifu mkubwa uliosababishwa na uvamizi wa Israel kwenye vitongoji vya makazi, misikiti na shule huko Gaza. Ushahidi wa karibuni zaidi ni picha ya angani ya kambi ya Jabalia, inayoonyesha mashambulizi makali ya kufuta kabisa makazi ya raia na kiwango kikubwa cha maangamizi ya kambi hiyo.

Picha hiyo ya maangamizi ya Israel imeakisiwa kwa kiwango kikubwa katika mitandao ya kijamii, huku wadau wakitoa maoni mbalimbali kuhusu shambulizi hilo ambalo picha zake zinaonyesha wingu zito la moshi uliotanda eneo lote la makazi ya raia, ikiwa ni ishara kuwa eneo hilo limegeuka kuwa majivu.

Akitoa maoni yake kuhusu shambulizi hilo, mlinganiaji wa Kipalestina Jihad Hals ameandika ujumbe kwenye jukwaa la “X” kwamba: “Hili sio bomu la nyuklia lililodondoshwa Hiroshima. Huu ni mji wa Jabalia, ambao sasa unaangamizwa mbele ya macho ya dunia nzima .”

Jabalia, Hiroshima ya Gaza

Mwandishi wa habari wa Kipalestina, Muhammad Hamdan, yeye ameandika: “Moshi ulipanda juu, ukibeba majivu ya watu na mawe, na kumbukumbu na ndoto zetu zimeyeyuka. “Hakuna kinachoweza kuhalalisha ukatili huu, hakuna kinachofanana nao, na hakuna kinachoweza kufidia.”

Wachambuzi wengi wanaamini kuwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametumia fursa ya walimwengu kushughulishwa na uchaguzi wa rais wa Marekani kutekeleza awamu hatari zaidi ya mauaji ya kimbari kaskazini mwa Gaza, na kuwalazimisha wakazi wa kaskazini kukimbia nyumba zao kwa lengo la kudhibiti ardhi hiyo kwa kisingizio cha “usalama.”