
Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, imeeleza kuridhishwa na mfumo wa ununuzi wa bando la tozo kwa ajili ya matumizi ya Daraja la Nyerere, Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Imesema watumiaji wa daraja hilo waendelee kulipia bando kwa kuwa ni nafuu, rahisi, hupunguza msongamano na huchangia ongezeko la mapato.
Akizungumza leo Jumanne Novemba 12, 2024 jijini hapa wakati wa kuhitimisha ziara ya kamati hiyo iliyokuwa ikitembelea miradi ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), likiwamo Daraja la Nyerere, mwenyekiti wa kamati hiyo, Fatma Toufiq amesema NSSF ilifikiri vema kuanzisha mfumo huo wa malipo kwa bando. “Tunaipongeza Serikali na wenzetu wa NSSF kwa kazi nzuri sana iliyofanyika kwenye Daraja la Nyerere; kuwepo kwa mifumo hii kunapunguza msongamano na pia upotevu wa mapato,” amesema Fatma.
Amesema kamati hiyo inaishukuru Serikali na Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada za kuleta maendeleo nchini ambayo ni manufaa ya wananchi.
Mwenyekiti huyo amesema kamati hiyo inaunga mkono juhudi zote za Serikali huku ikiamini NSSF itaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa wanachama wake kupitia uwekezaji wake.
Mjumbe wa kamati hiyo, Katani Katani pamoja na kuunga mkono mfumo huo wa ununuzi wa bando katika daraja hilo, amewahimiza wananchi kujiunga na kutumia mfumo huo kwa kuwa ni rahisi na unapunguza msongamano. Mbunge Mariam Kisangi akizungumzia mradi huo, amesema umeendelea kuchochea maendeleo kwa wakazi wa Kigamboni na kuwataka wananchi kuendelea kulipia tozo kupitia bando ili kuondoa usumbufu.
Kwa upande wake, mbunge, Athumani Maige amewataka wananchi kuendelea kutumia malipo ya bando wanapopita darajani na akaipongeza NSSF kwa usimamizi bora wa mradi huo.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesisitizia umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya bando huku akibainisha kuwa ni njia rahisi inayopunguza usumbufu kwa watumiaji wa daraja hilo la Nyerere.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema wanaendelea kuwahamasisha watumiaji wa daraja hilo kuendelea kulipia bando la siku, wiki au mwezi kwa urahisi zaidi, akisisitiza kuwa ni nafuu.