Kamati ya kitaifa biashara ya kaboni yapewa majukumu

Dodoma. Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Biashara ya Kaboni nchini imepewa jukumu la kutathmini fursa na changamoto zinazoikabili biashara hiyo ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Kadhalika, kamati hiyo imepewa jukumu la kufanya tathmini na kutoa mapendekezo kuhusu njia bora na mwenendo wa biashara ya kaboni nchini, biashara ambayo imeonekana kufanyika kiholela huku Serikali ikiwa haipati mapato yoyote kutokana nayo.

Akizindua kamati hiyo Aprili 10, 2025 jijini Dodoma, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni, amesema kamati hiyo inaundwa na watu 20 kutoka wizara za kisekta, taasisi za umma, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Masauni amesema jukumu jingine la kamati hiyo ni kubaini na kuchambua changamoto za mfumo mzima wa biashara ya kaboni nchini kuanzia kwenye usajili, upimaji, uuzaji na makubaliano, ili kuongeza uwazi, ufanisi na uwajibikaji, pamoja na kuangalia masuala ya udhibiti wa biashara hiyo.

“Tunaitegemea kamati hii kutoa ushauri kuhusu biashara ya kaboni, hususan katika kupata taarifa sahihi zitakazosaidia nchi kunufaika zaidi na mapato yatokanayo na biashara hiyo.

Pia inatakiwa kushauri namna ambavyo maeneo yote muhimu ya kiuchumi yanaweza kufaidika na biashara ya kaboni, ikiwemo miradi mikubwa ya kimkakati kama vile Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (BRT) na Treni ya Mwendokasi (SGR),” amesema Masauni.

Amesisitiza kuwa kamati hiyo inapaswa kuchambua hali ya usimamizi wa biashara ya kaboni nchini na kutathmini mfumo wa ufuatiliaji na tathmini, kwa kuwa ni muhimu kuwa na mfumo madhubuti wa kufuatilia na kutathmini miradi ya kaboni ili kuhakikisha inaleta manufaa yaliyokusudiwa kwa mazingira, jamii na uchumi.

“Tunategemea mchango wenu katika kuhakikisha kuwa Tanzania inapata faida kutokana na fursa hizi za biashara ya kaboni,” alisema na kuongeza:

“Nisisitize kuwa nategemea kupata taarifa ya tathmini ya hali ya usimamizi wa biashara ya kaboni na mapendekezo ya njia bora na mwenendo wa biashara hiyo nchini ndani ya mwezi mmoja kutoka leo. Naomba mjipange kadri inavyowezekana, ikiwemo kuunda kamati ndogo ndogo na kupeana majukumu mahususi.”

Alisema Serikali itaendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi na biashara ya kaboni kwa kutumia mbinu bora zinazozingatia maslahi ya kitaifa na kimataifa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Hamad Masauni akizungumza na wajumbe wa kamati ya Kitaifa ya ushauri kuhusu biashara ya kaboni wakati akizindua kamati hiyo Jijini Dodoma

Kwa mujibu wa Masauni, uzinduzi wa kamati hiyo ni hatua muhimu katika mwelekeo wa kusimamia na kuratibu biashara ya kaboni nchini kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamza Hamis Hamza, alisema kamati hiyo pia ina jukumu la kutoa elimu kwa wananchi ili wajue fursa zinazopatikana kupitia biashara ya kaboni, ili kwa pamoja waweze kushiriki kikamilifu katika biashara hiyo.

Alisema biashara hiyo inaweza kuongeza pato la taifa kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo tayari zimeanza kunufaika nayo, hivyo fedha zitakazopatikana zitachangia kugharamia huduma za kijamii.

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Cyprian Luhemeja alisema kamati hiyo imeundwa kwa lengo la kuchambua fursa zilizopo katika biashara ya kaboni ili taifa lianze kunufaika na biashara hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *