Arusha. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeitaka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kutangaza na kusambaza ubunifu wake wa kiteknolojia ili ufanikishe malengo ya kuleta manufaa kwa jamii ya Watanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.
Licha ya NM-AIST kuwa na uwezo mkubwa katika kukuza ubunifu wa kiteknolojia, kumekuwa na changamoto ya kutokuwa na mikakati madhubuti ya kutangaza na kueneza ubunifu huo kwa manufaa ya wananchi.
“Ni muhimu kwa taasisi kama NM-AIST kuwa na mbinu za kutangaza na kusambaza ubunifu wake kwa jamii, ili teknolojia zinazozalishwa na wataalamu wetu ziweze kutumika katika kutatua changamoto za kijamii, kiuchumi, na kiutamaduni,” alisema Mjumbe wa kamati ya PAC na mbunge wa Momba, Condester Sichwale.
Sichwale amesema NM-AIST inatekeleza kazi kubwa ya kufanya tafiti na kubuni teknolojia za kutatua changamoto katika jamii, lakini zinashindwa kuwa na tija kutokana na kuishia kwenye makabrasha.

“Bunifu ni nzuri na Teknolojia tumeona ni nyingi na nzuri, lakini hazina tija kama zitabaki kwenye makabrasha yenu bila kufikia jamii na kutumika kwa manufaa ya wananchi hivyo niwaomba hakikisheni zinasambaa na kufikia walaji hapo ndio mtafiti au mbunifu atapata faida ya kiuchumi, lakini pia furaha kutatua shida husika,” amesema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya PAC, Josephat Hasunga ameitaka taasisi hiyo kuhakikisha kila tafiti na bunifu wanayoifanya wanaitangaza ili walaji wapate kuzijua na kuzichangamkia.
“Kuna mahali hadi sasa wanateseka na mimea vamizi kwenye mazingira yao kumbe nyie mnayo bunifu ya kuhakikisha mnakabiliana nayo, lakini mmekaa nayo tu, hivyo kuanzia sasa hakikisheni mnafanya matangazo na kusambaza,” amesema.
Mbali na hilo aliwataka kutimiza ndoto ya Nelson Mandela ya kuasisi taasisi hiyo katika kuhakikisha Afrika zinajitegemea kwa gunduzi na teknolojia zake bunifu.
Pia, aliwataka kuhakikisha wanaendelea kufanya utafiti nyingi na kuleta ubunifu zenye kutatua changamoto zinazoikumba jamii na kusambaza mapema kabla ya kupitwa na teknolojia mpya.
“Fanyeni bunifu nyingi kadri muwezavyo maana bado jamii ina changamoto nyingi na inategemea ninyi watafiti kuleta suluhu na hii inataka kuharakisha usambazaji wake kabla haijapitwa na wakati kwa bunifu na teknolojia za nje zinazoingia kila kukicha,” amesema.
Wajumbe wa kamati hiyo walitoa ushauri huo leo, Machi 25, 2025, walipotembelea mradi wa ujenzi wa hosteli ya wanafunzi yenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 184 katika Taasisi ya NM-AIST, iliyoko mkoani Arusha.
Ushauri wa kamati hii unakuja baada ya taarifa ya Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST, Profesa Maulilio Kipanyula, kuonyesha kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuzalisha bunifu 110, ingawa hadi sasa bunifu mbili pekee ndizo ziko sokoni.
Profesa Kipanyula alisema kuwa, kati ya bunifu hizo, 22 zina hati miliki, sita zimeshapata idhini ya kutangazwa, mbili ziko katika mchakato wa marekebisho, na nne zinapitia tathmini ili ziingie sokoni.
Akielezea baadhi ya bunifu zilizozalishwa na taasisi hiyo, Profesa Kipanyula alitaja kifaa mseto cha kukausha mazao kwa kutumia nishati ya jua na biogas, pamoja na mbinu ya kukausha mazao ya kilimo.
Pia, alielezea ubunifu wa dawa ya asili ya mimea inayoweza kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) na magonjwa ambukizi (CDs).
“Ubunifu mwingine ni mashine ya kiroboti ya kuchukua na kuweka vitu katika sehemu maalumu, inayojulikana kama ‘Indu-Acad Robo AivisioInspect Robotic Arm,’ pamoja na bunifu zingine nyingi” amesema.
Akizungumzia ujenzi wa bweni hilo, mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya NM-AIST, Balozi Maimuna Tarishi amesema kuwa ujenzi wa bweni hilo ulioanza 2021 limefikia asilimia 74 ambapo hadi kukamilika kwake June 30, 2025 utagharimu jumla ya Sh6.1 bilioni kwa ajili ya kulaza jumla ya wanafunzi 184.
Amesema ujenzi huo unaojengwa kwa mfumo wa ‘force account’ ni utekelezaji wa malengo na taasisi ya kuongeza idadi ya wanafunzi kutoka 600 mwaka 2021 hadi kufikia 1000 mwaka 2026.
“Kwa sasa tuna jumla ya wanafunzi 802 wakiwemo wa kigeni 83 kutoka mataifa 16 duniani,” amesema.
Amesema taasisi hiyo inayopokea wanafunzi wa shahada ya umahiri na uzamivu pekee imejikita katika kufanya tafiti na bunifu mbalimbali za kusaidia jamii kutatua changamoto wanazokumbana nazo katika nchi zote za Afrika.
“Taasisi yetu itaendelea kuwa na bunifu nyingi na kuzilinda ikiwemo zile za kusaidia maendeleo ya viwanda katika nchi za Afrika ili kunufaika katika kuzibiasharisha lakini pia jamii isaidike,” amesema.