
Kamanda Mkuu wa zamani wa Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameonya kuwa utawala wa Israel na washirika wake wataanza kuzilenga kijeshi nchi muhimu za eneo la Asia Magharibi ikiwemo Iran ikiwa watafanikiwa katika vita vyao vya sasa dhidi ya mataifa ya Palestina na Lebanon.
Meja Jenerali Mohsen Rezaei, ambaye kwa sasa anahudumu katika Baraza la Kuainisha Mslahi ya Jamhuri ya Kiislamu, alisema Jumanne kwamba: “Suala kuu katika vita ni Iran.”
“Katika suala hili, Gaza na Lebanon zimegeuka kuwa mstari wa mbele wa ulinzi kwa nchi zote za Asia Magharibi,” alisema na kuongeza, “Ikiwa Gaza na Lebanon zitaanguka, adui ataanza kuelekea Syria, Iraq, Saudi Arabia, Uturuki na Iran.”
Matamshi hayo yametolewa wakati utawala haramu wa Israel unaendeleza mauaji ya kimbari huko Gaza na Lebanon. Tokea Oktoba mwaka jana jeshi katili la Israel limeua Wapalestina wasiopungua 44,000 wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto na kuuwa watu wengine 3,544 wa Lebanon.
Mashambulizi hayo ya kikatili ya kijeshi yamekuwa yakipata uungwaji mkono kamili wa kisiasa, kijeshi na kijasusi wa Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya.