Behrouz Kamalvandi, msemaji na mkuu wa masuala ya kimataifa na kisheria katika Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amezungumzia azimio haribifu la Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) dhidi ya Iran na kusema: Tumeongeza kwa kiasi kikubwa uwezo wa kurutubisha madini ya urani.
Usiku wa Alhamisi, azimio lililopendekezwa na nchi tatu za Ulaya, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani pamoja na Marekani dhidi ya miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani nchini Iran, liliidhinishwa na Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Kamalvandi ameongeza kuwa: “Nchi za Magharibi zinajaribu kurudisha nyuma sekta ya nyuklia ya Iran, lakini kamwe hazitafanikiwa.”
Msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameendelea kusema kwamba, kura za kuunga mkono azimio jipya dhidi ya Iran ni ndogo sana kuliko ilivyokuwa katika vikao viliyotangulia. Amesema: “Kama ilivyosisitizwa wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu IAEA nchini Iran, Alhamisi usiku wakati azimio hili lilipopitishwa katika saa za mwisho na kabla ya maafisa wa IAEA kuondoka kwenye ukumbi wa mkutano, Iran tayari ilikuwa imeanza kuchukua hatua za kukabiliana na azimio hilo.”

Mapema Ijumaa, Wizara ya Mambo ya Nje na Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran zilitoa taarifa ya pamoja na kusema: “Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ametoa amri ya kuchukuliwa hatua madhubuti za kuwekwa majimui maalumu ya mashinepewa (centrifuges) mpya na za kisasa za aina tofauti.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imesema: Ni wazi kwamba, hatua hizo zinatekelezwa kwa lengo la kulinda maslahi ya Iran na kustawisha zaidi kadiri iwezekanavyo sekta ya nyuklia yenye malengo ya amani, kwa mujibu wa mahitaji ya kitaifa yanayozidi kuongezeka na ndani ya fremu ya haki na majukumu ya Iran kwa mujibu wa makubaliano kamili ya usimamizi; na wakati huohuo ushirikiano wa kiufundi na kiusimamizi na IAEA utaendelea kama ilivyokuwa awali na kulingana na hati ya makubaliao ya usimamizi.