Kama wewe unatumia iPhone hili linakuhusu

Dar es Salaam. Kama wewe ni mtumiaji wa iPhone na vifaa vingine vya kampuni ya Apple hili linakuhsu, unadhani serikali inapaswa kuwa na uwezo wa kufikia taarifa zako binafsi, au Apple inapaswa kuendelea kulinda faragha ya watumiaji?

Mwishoni mwa wiki, Apple imeondoa zana yake ya juu zaidi ya ulinzi wa taarifa (Advanced Data Protection – ADP) nchini Uingereza baada ya serikali kudai haki ya kuona data, Mtandao wa Dailymail umeripoti.

Kuondolewa kwa ADP Uingereza kunaibua maswali kuhusu usalama wa data na haki ya faragha.

ADP inayolinda data iliyohifadhiwa kwenye iCloud kwa usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho, inamaanisha kuwa data hiyo inaweza kuonekana na mmiliki wake.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Apple, Tim Cook amesema, “Hatuwezi tena kutoa ADP nchini Uingereza kwa watumiaji wapya na watumiaji wa sasa watalazimika kuzima kipengele hiki cha usalama.”

“Tunavunjika moyo sana kuwa ulinzi unaotolewa na ADP hautapatikana kwa wateja wetu nchini Uingereza ikizingatiwa kuendelea kuongezeka kwa uvujaji wa taarifa na vitisho vingine kwa faragha ya wateja.”

Ikiwa unatumia iPhone, mabadiliko haya yana athari gani kwa taarifa zako binafsi?

ADP ni kiwango cha juu zaidi cha ulinzi wa taarifa za iCloud kutoka Apple, ambacho kinalinda data yako kwa usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho.

Hii inamaanisha kuwa hakuna mtu mwingine anayeweza kufikia taarifa zako, hata Apple yenyewe na taarifa zako zinabaki salama hata kama kuna uvunjaji wa usalama wa iCloud.

Hata hivyo, Apple sasa imeondoa ADP kwa watumiaji wapya nchini Uingereza, kufuatia ombi kutoka kwa serikali mapema mwezi huu.

“Kuimarisha usalama wa uhifadhi wa wingu kwa usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho ni muhimu zaidi kuliko wakati wowote,” Msemaji wa Apple amesema.

Apple imesema ina matumaini kuwa itaweza kutoa kiwango hiki cha usalama tena nchini Uingereza siku zijazo.

Hii inamaanisha nini kwa watumiaji wa iPhone?

Kwa bahati nzuri, kuondolewa kwa ADP hakutaathiri kategoria 14 za data za iCloud ambazo tayari zina usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho kwa chaguo msingi na kategoria tisa za data sasa zitalindwa tu kawaida, bila chaguo la usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho.

“Apple haina funguo za usimbaji fiche kwa kategoria hizi na hatuwezi kukusaidia kurejesha data hii ukipoteza ufikiaji wa akaunti yako,” Apple imeeleza kwenye tovuti yake. Hata hivyo nje ya Uingereza, ADP bado inapatikana kila mahali.

Mapema mwezi huu, serikali ya Uingereza ilidai kuwa na uwezo wa kufikia data iliyo kwenye cloud ya watumiaji wa Apple.

Ombi hili lilitolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani chini ya Sheria ya Mamlaka ya Upelelezi (Investigatory Powers Act – IPA), ambayo inazilazimu kampuni kutoa taarifa kwa vyombo vya sheria.

Apple imeeleza mara kwa mara kuwa haitawahi kuunda “mlango wa nyuma” au “funguo kuu” kwa bidhaa au huduma zake.

Uamuzi huo umepokelewa kwa hisia tofauti. Wapo wanaounga mkono hatua ya serikali akiwemo Rani Govender, Meneja wa Sera ya Usalama wa Mtoto Mtandaoni NSPCC.

Govender anasema “Usimbaji fiche wa mwisho hadi mwisho unawapa wahalifu fursa ya kuwanyanyasa watoto bila kugundulika. Apple inapaswa kuhakikisha inachukua hatua nyingine za kulinda watoto mtandaoni”

Hata hivyo wapo wanaopinga hatua ya serikali, akiwemo Mshauri wa usalama wa mtandao kutoka ESET, Jake Moore ambaye anasema “Uamuzi huu ni pigo kubwa kwa faragha na usalama wa data. Uundaji wa mlango wa nyuma kwa sababu za kimaadili utatoa mwanya kwa wadukuzi pia”

Kwa miaka mingi watumiaji wa IOS wakiwemo wamiliki wa simu za iPhone usalama ni mzuri iwapo mtumiaji ataihuisha simu yake ‘update IOS’ mara kwa mara.

Herieth Makwetta na Mashirika