
Dar es Salaam. Kocha wa KMC, Kally Ongala amesema kuwa anafurahishwa na mwenendo wa timu yake katika mechi alizoiongoza kwenye Ligi Kuu huku akiwataka wachezaji wake kutobweteka katika mechi 12 walizobakiza msimu huu na badala yake wanapaswa kujituma zaidi kwa vile ligi ni ngumu.
Ongala ametoa kauli hiyo siku mbili baada ya KMC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Singida Black Stars ulioifanya timu yake kusogea hadi nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 22.
Ongala amesema kuwa wachezaji wa KMC wanatakiwa kuwa na muendelezo wa ushindi na kucheza vizuri kwani hiyo ndio njia pekee ambayo itawafanya wasogee juu kwenye msimamo wa ligi.
“Timu inaimarika inacheza vizuri. Kuna wakati tunaangusha pointi tatu lakini mimi na wachezaji wangu tunajua tunaimarika wapi na tunafanyia kazi kitu. Tuko kwenye kiwango bora.
“Mzunguko wa pili ni mgumu kwa sababu kila mtu hataki kushuka daraja na hasa ukienda ugenini kila timu inataka kushinda nyumbani, kuna mambo mengi sana. Kitu ambacho tunafanya kama timu hatuwezi kuhangaika na wapinzani kujua wanafanya nini zaidi ni kuangalia timu yetu inachezaje,” alisema Ongala.
Kocha huyo alisema nafasi waliyopo sio salama sana na kwa daraja la heshima kwa timu hiyo ni kutoka walipo na kumaliza katika nafasi za juu.
“Mechi 12 ni nyingi na lolote linaweza kutokea hivyo bado hatuko salama sana. Ili kutojiweka kwenye presha hapo baadaye ni lazima tuwe na muendelezo wa kufanya vizuri katika michezo iliyobaki ambayo kama usipojipanga vyema unaweza ukaanguka,” alisema Ongala.
KMC ambayo imecheza michezo 18, imeshinda mechi sita, sare nne na kupoteza nane inajiandaa kuvaana na Yanga kesho kwenye mchezo mgumu wa ligi hiyo.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 46, moja nyuma ya Simba iliyopo kileleni na pointi 47.