
LICHA ya kushindwa kubebwa na rekodi ya kupata matokeo mazuri mechi za ugenini Ligi Kuu Bara, kocha wa KMC, Kally Ongala amesema ametafuta dawa ya kupata matokeo mechi saba zilizobaki huku akiwa na michezo mitano ugenini na miwili nyumbani.
KMC ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo ikiwa na pointi 24 katika mechi 23 ilizocheza ikishinda sita, sare sita na kufungwa 11, imefunga mabao 16 na kufungwa 34 ambapo wameshinda mechi moja ugenini na sare tatu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kally alisema amefanyia kazi upungufu kwa kucheza mechi mbili za kirafiki na kubaini kikosi chake kipo katika hali nzuri ya utimamu wa mwili na pia kimepunguza makosa kwenye ulinzi na kuwa bora eneo la ushambuliaji.
“Tumecheza na Azam FC tumeshinda mabao 4-0, lakini pia tumecheza na Simba tumepoteza kwa mabao 3-0. Hii imenipa picha nzuri kuwa kuna mabadiliko ya uchezaji na naamini bado nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha naiweka timu kwenye nafasi nzuri ya kupata matokeo kwenye mechi saba ngumu zilizo mbele yetu,” alisema.
“Ni kweli sina matokeo mazuri ugenini na nina mechi nyingi za ugenini hilo haliniondoi kwenye mstari kuhakikisha naipambania KMC inapata nafasi ya kucheza tena ligi msimu ujao. Nawaheshimu wapinzani tunaotarajia kukutana nao natambua na wao wanahitaji matokeo dakika 90 zitaamua ubora.”
Kally ambaye alijiunga na KMC katikati ya msimu, alisema wachezaji wake wapo kwenye hali nzuri ya utimamu na wamemuahidi kuipambania nembo ya timu kuhakikisha wanacheza ligi msimu ujao.
Katika mechi 23 walizocheza nyumbani wameshinda tano huku wakishinda moja pekee ugenini, sare tatu ilhali nyumbani sare mbili huku wakifungwa mechi tano na ugenini wamepigika mara sita.
Kally alikabidhiwa kikosi Novemba 14, 2024 akichukua mikoba ya Abdihamid Moallin aliyetimkia Yanga.
Tangu ameanza kuiongoza timu hiyo, kocha huyo ameisimamia katika mechi 12 na kati ya hizo ameshinda michezo miwili dhidi ya Singida Black Stars akiiongoza kushinda mabao 2-0 na Pamba Jiji akiifunga bao 1-0, huku akiwa na sare nne na vipigo sita akiwa amefungwa mabao 18 akiiongoza kufunga mabao manane.