Dar es Salaam. Wikiendi hii mwanamitindo, Hamisa Mobetto na mchezaji wa Yanga SC, Aziz Ki wana jambo lao baada ya kile kinachotajwa kuwa walishafunga ndoa na sasa wanaenda kuweka kila kitu wazi kwa mashabiki wao.
Hata hivyo, baadhi ya vyanzo ndani vinadai kuwenda wawili hao wakatambulisha reality show yao ambayo itaanza kuruka katika moja ya vituo vya runinga nchini muda sio mrefu.
Kutokana na ushawishi walionao katika tasnia ya burudani na michezo, tunakuletea kalenda ya matukio ya Hamisa na Aziz Ki ambayo kwa ujumla yametufikisha hapa tulipo.
Mei 20, 2024: Wanaonekana pamoja JNIA
Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kwa wawili hao kuonekana pamoja, ni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Hamisa alikuwa katikati ya kundi la wachezaji wa Yanga waliotua uwanjani hapo.
Hata hivyo, Aziz Ki pekee ndiye aliyekuwa na akizungumza na Hamisa ambaye alionekana kuwa na wasiwasi kiasi na kuanzia hapo tetesi za wawili hao kutoka pamoja zikaanza kuchukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii.

Juni 10: 2024: Hamisa anamkana Aziz Ki
Baada ya kulamba dili fulani la ubalozi, Hamisa anafanya mahojiano na kukanusha vikali kutoka na Aziz Ki na kusema yeye yupo singo na ilitokea tu akajikuta amepanda ndege moja na Yanga ila sio sababu ya mchezaji hiyo.
Alidai wao ni marafiki tu na yeye bado ni shabiki wa Simba SC ingawa mama yake, dereva wake na watu wake wengi wa karibu wanaomzunguka ni mashabiki wa Yanga, hivyo sio ajabu kuwa karibu na wachezaji wa timu hiyo akiwemo Aziz Ki.
Julai 11, 2024: Wanaisimamisha Instagram
Kwa mara ya kwanza wanachapisha picha na video zao mtandaoni na kuendelea kukoleza tetesi za kuwa pamoja katika penzi licha ya Hamisa kukanusha hapo awali, na kuanzia hapa mambo yakachangamka sana.
Video ambayo walishirikishana (collab post) katika kurasa zao za Instagram, iliwaonyesha wakiwa uwanjani ambapo Aziz Ki alionyesha uwezo wake wa kuchezea mpira na baadaye alisimama golini huku Hamisa akipiga penalti.
Katika video hiyo Aziz Ki aliandika; new striker in town – akimaanisha, mshambuliaji mpya mjini. Chapisho hilo lilivutia watu wengi na hadi sasa likiwa limepokea maoni (comments) zaidi ya 10,000 na kutazamwa (views) zaidi ya mara milioni 3.7.

Baadhi ya maoni ya mashabiki katika chapisho hilo yalimpongeza Hamisa kwa kile walichodai ndiye alisababisha mchezaji huyo kusaini mkataba mpya ndani ya Yanga baada ya kuwepo tetesi za kutimkia Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.
Agosti 1, 2024: Wanaongozana tuzo za TFF
Katika tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ajili ya kuwatunza waliofanya vizuri msimu wa 2023/24, wawili hao waliongozana katika hafla hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa The Super Dome, Masaki.
Walitumia jukwaa la tuzo hizo kuonyesha ni kiasi gani uhusiano wao umepiga hatua kubwa, hiyo ni baada ya Aziz Ki kushinda tuzo tatu, akishinda ile ya Mfungaji Bora, Kiungo Bora na Mchezaji Bora Ligi Kuu (MVP).
Kutokana na kushinda tuzo ya MVP, Aziz Ki alipewa zawadi na mdhamini wa Ligi Kuu ya kwenda kupumzika Dubai siku tano na kulala siku nne pamoja na mwenza wake kitu kilichoibua shangwe ukumbini hapo.
Akiwa jukwaani, Aziz Ki aliulizwa na MC wa shughuli hiyo kama ataenda Dubai na mpenzi wake, naye alijibu ataenda. Je, ni nani huyo, jibu ni Hamisa ambaye alikuwepo karibu yake. Hamisa alionyesha kufurahia safari hiyo ambayo haikuweka wazi itakuwa lini hasa.

Agosti 4, 2024: Aziz Ki anamkaribisha Hamisa Yanga
Katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, Aziz Ki alitumia juwaa hilo kumvisha Hamisa jezi ya Yanga ikiwa ni ishara ya kumkaribisha katika timu hiyo kama shabiki akitokea Simba ambapo alishiriki mambo mengi makubwa.
Hamisa alikuwa shabiki wa Simba kwa miaka, mathalani Januari 30, 2021 katika fainali ya Simba Super Cup, shindano dogo la kirafiki liloshirikisha na timu nyingine kama Al Hilal ya Sudan na TP Mazembe ya DR Congo, Hamisa ndiye aliyeleta kombe uwanjani.
Novemba 7, 2024: Hamisa anashuhudia Aziz Ki akikosa penalti
Ilikuwa jioni moja tulivu ambapo Hamisa alienda uwanja wa Azam Complex kutazama mchezo wa Ligi Kuu uliowakutanisha Yanga SC dhidi ya Tabora United lakini isivyo bahati timu yake iliambulia kipigo cha magoli 3-1.
Mbaya zaidi alishuhudia mpenzi wake Aziz Ki akikosa mkwaju wa penalti katika mchezo huo ambao ulikuwa ni wa pili mfululizo kwa Yanga kupoteza katika Ligi msimu wa 2024/25 baada ya hapo awali kutandikwa na Azam FC goli 1-0.
Desemba 10, 2024: Wanathibitisha kuchumbiana
Akisherehekea kutimiza umri wa miaka 30 hapo Desemba 10, 2024, Hamisa alichapisha picha yake Instagram ikiwa imepambwa na kalenda na ndipo akathibitisha yeye na Aziz Ki tayari ni wachumba.
Hiyo ni baada ya Aziz Ki kutoa maoni yake kwa lugha ya Kifarasa katika picha hiyo ya Hamisa akisema; “Maisha yenye furaha kuwa na furaha milele na nuru, heri ya kuzaliwa mchumba. Kisha akamalizia na emoj ya busu!.
Hamisa ambaye alizaliwa mwaka 1994 huko Mwanza akiwa mtoto pekee kwa mama yake, hakuwa nyuma kuujibu ujumbe huo wa Aziz Ki, naye alitumia lugha ya Kifaransa akiandika; Merci mon fiancé – akimaanisha, asante mchumba wangu.

Januari 15, 2025: Aziz Ki anamshukuru Hamisa kwa zawadi
Baada ya ukimya wa muda kiasi bila penzi lao kugonga vichwa habari Bongo, Aziz Ki anaibuka kupitia Insta Story na kumshukuru Hamisa kwa kumnunulia viatu vya kuchezea mpira ili aendelee kuwapa raha mashabiki wa Yanga.
Aziz Ki aliyetua Yanga hapo Julai 2022 baada ya kuonyesha uwezo mkubwa pale ASEC Mimosas ya Ivory Coast, alichapisha picha ya viatu hivyo na kuandika; asante Boss, kisha kumtag Hamisa ambaye baadaye alijibu kwa kusema, karibu.
Baadaye Hamisa alikuja kusema viatu alivyompa Aziz Ki vilikuwa ni pea tatu na vilinunuliwa Afrika Kusini katika duka la Puma ingawa alikataa kutaja bei yake huku akisema anafanya hivyo kwa lengo la kumshika mkono katika kazi yake.
Januari 29, 2025: Wanathibitisha kwenda Dubai
Kama walivyoweka wazi katika tuzo za TFF mwaka uliopita, ni kweli Aziz Ki na Hamisa walikuja kwenda kupumzika huko Dubai ingawa bado haijajulikana ni lini hasa ndege hao wapendanao walipaa kuelekea huko.
Mnamo Januari 29, 2025, wote walichapisha picha zao Instagram zikiwaonyesha wakiwa ndani ya boti Dubai huku Hamisa akitoa neno zuri la upendo kwa Aziz Ki akisema; Yeye ndiye hasa shairi ninalotaka kuandika.
Februari 9, 2025: Wanapita aga za Jay Z na Beyonce
Wakati picha zao zikiendelea kuwa gumzo, Hamisa na Aziz Ki wanarejea tena Instagram wakichapisha video ya bata lao huko Dubai na kusindikizia na wimbo wa rapa wa Marekani, Jay Z akimshirikisha mkewe Beyonce Knowles, Part II (On The Run).
Utakumbuka Jay Z na Beyonce ambao uhusiano wao ulianza mwishoni mwa miaka ya 1990, ni miongoni mwa mastaa wanandoa wenye nguvu kubwa ya ushawishi duniani huku utajiri wao ukikadiriwa kufikia Dola3.3 Bilioni.
Walipotoa kolabo yao ya kwanza, 03 Bonnie & Clyde (2002) ndipo akathibitisha kuwa ni wapenzi, walifunga ndoa mwaka 2008 na kujaliwa mtoto wao kwanza, Blue Ivy hapo Januari 2013, kisha pacha, Sir na Rumi (2017). Je, Aziz Ki na Hamisa watafikia huku?.
Februari 11, 2025: Mama Hamisa anathibitisha ndoa yao!
Akiongea na kipindi cha Leo Tena kinachoruka Clouds FM, mama mzazi wa Hamisa alidai kuwa mwanae na Aziz Ki walishafunga ndoa muda mrefu takribani miezi minne iliyopita na waliodhuria ni watu wachache.
Mama Hamisa alienda mbali zaidi na kudai sehemu ya watu kutoka kwa mdhamini wa Yanga, GSM ndio walioleta posa nyumbani kwake kisha ndoa kufungwa kimya kimya, hivyo shughuli inayofuata ni kama kuweka jambo hilo rasmi kwa umma.
Je, kalenda Hamisa inasemaje?
Kuwa na uhusiano na Aziz Ki sio mara ya kwanza kwa Hamisa kugonga vichwa vya habari, amefanya hivyo kwa miaka nenda rudi akiwa kama mlimbwende, mwanamitindo, mwanamuziki n.k, na hii ndio kalenda yake.
1. Desemba 2010 – Hamisa anashinda taji la Miss XXL After School Bash akitokea sekondari ya Tandika, Dar es Salaam. Baadaye anaibuka mshindi wa pili Miss Dar Indian Ocean 2011, nusu fainali ya Miss Tanzania 2011 na 10 bora ya Miss University Africa 2012.
2. Aprili 2012 – Hamisa anatokea katika video yake ya kwanza ya muziki kama vixen, ni katika wimbo wa Barnaba, Magubegube (2012), kisha vinafuata video za wasanii wengine kama Quick Rocka, My Baby (2013), Diamond, Salome (2016) n.k.
3. Aprili 2015 – Hamisa anajifungua mtoto wake wa kwanza, Fantasy, wakati huo alikuwa katika uhusiano na Mkurugenzi Mtendaji wa E FM Radio na TV E, Francis Ciza maarufu kama Majizzo ambaye sasa ni mume wa muingizaji Elizabeth ‘Lulu’ Michael.
4. Septemba 2016 – Hamisa anahusishwa kuwa na uhusiano na Diamond baada ya kuonekana katika video ya wimbo wa msanii huyo, Salome (2016) ingawa wote wawili wanakanusha vikali jambo hilo.
5. Agosti 2017 – Hamisa anajifungua mtoto wa pili na kumpa jina la Dylan lakini suala la ni nani baba mtoto linabaki kuwa siri yake huku kukiwa na maneno mengi katika mitandao yanayomtaja Diamond kuwa ndiye baba mtoto.
6. Septemba 2017 – Diamond anakiri hadharani kuwa yeye ndiye baba wa mtoto huyo wa pili wa Hamisa na kuomba msamaha kwa aliyekuwa mpenzi wake na mzazi mwenzie, Zari The Bosslady kwa yote yaliyotokea na kusema yupo tayari kuwajibika.
7. Agosti 2018 – Hamisa anatoa wimbo wake wa kwanza kama mwanamuziki ‘Madam Hero’ ambao uliandikwa na Foby na C 9, Januari 2019 anafanya show ya kwanza, kisha Mei 2022 anatoa EP yake ya kwanza ‘Yours Truly’ yenye nyimbo sita.
8. Novemba 2021 – Hamisa na rapa wa Marekani wanaonekana pamoja Dubai baada ya ukaribu wao miezi kadhaa nyuma katika mitandao huku akitajwa kuwa na uhusiano lakini baadaye walikuja kuonekana katika tangazo la kampuni ya simu.
9. Septemba 2023 – Hamisa anatambulisha mpenzi wake mpya, Kevin Sowax kutokea Togo ambaye alikuja nchini na wote kufika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kutoa msaada kwa watoto wadogo wanaopambana na ugonjwa wa saratani.
10. Juni 2024 – Hamisa anasema licha ya kuachana na Kevin Sowax hakuna anachojutia maana ulikuwa uamuzi sahahi kwake kuwa naye na ni mahusiano aliyoyafurahia sana, na wakati huo ndio alikuwa ameanza kuhusishwa na Aziz Ki kutokea Burkina Faso.