
KIUNGO wa Simba, Yusuf Kagoma na beki wa kulia wa Yanga, Israel Mwenda ni miongoni mwa wachezaji waliothibitisha kushiriki tamasha la Alliance Day litakalotumika kumuenzi aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, James Bwire aliyefariki dunia mapema mwaka huu.
Uongozi wa kituo hicho cha michezo cha Alliance kilichopo jijini hapa umetangaza ujio wa tamasha hilo ili kuenzi maono na kusherehekea maisha ya mwasisi, James Bwire, katika kuunganisha familia ya soka kwa waliowahi kupita kituoni hapo pamoja na wanafunzi waliowahi kusoma katika shule za Alliance.
Tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika Julai 9, 2025 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza litawakutanisha wachezaji na mastaa mbalimbali wa soka waliopo ndani na nje ya nchi waliokuzwa kituoni hapo akiwamo Yusuph Kagoma (Simba), Novatus Dismas (Goztepe), Israel Mwenda (Yanga), Hans Masoud (KMC), Mapinduzi Balama (Mashujaa) na Zabona Mayombya (Pamba Jiji).
Wengine ni Juma Nyangi (Mtibwa Sugar) na Aisha Masaka (Brighton – England), Aisha Mnunka (Simba Queens) na Enekia Kasonga (Femenil Club Mazatlan), ambapo litahusisha mechi ya soka ya mastaa wa Alliance (Alliance All Stars) dhidi ya timu pinzani itakayotangazwa hapo baadaye.
James Bwire ambaye ni mwasisi wa kituo cha michezo cha Alliance kilichopo Mahina jijini Mwanza kinachomiliki timu za Alliance FC iliyoanzishwa mwaka 2012 na kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2018/19, na Alliance Girls inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake, alifariki usiku wa kuamkia Januari 26, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando na kuzikwa kijijini kwao Nyamwaga, Tarime Februari 2, mwaka huu.
Mratibu wa tamasha hilo, Nelson Marwa alisema lengo ni kusherehekea maono na maisha ya mzee Bwire, kuita wadau, wawekezaji, marafiki na familia ya Alliance pamoja.”