
STRAIKA wa Namungo, Mnyarwanda Meddie Kagere (MK 14 the Terminator), amesema tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara msimu wake bora ni ule wa kwanza 2018/19 ambao alimaliza na mabao 23 – akichangia zaidi ya robo ya mabao 62 ya Simba.
Katika msimu huo Simba ilikuwa bingwa ikiwa na pointi 93, ikimaliza na mabao 62 ambapo 39 yalifungwa na wachezaji wengine huku 23 yakifungwa na Kagere.
“Ulikuwa ni msimu wa ushindani wa hali ya juu kuanzia katika kikosi hadi kwa washambuliaji wa timu nyingine ambao walikuwa wananipa chachu ya kupambana zaidi, nikafanikiwa kuchukua kiatu cha dhahabu, lakini wengi walifunga mabao mengi,” alisema Kagere.
“Msimu huo Simba ilikuwa na kikosi bora sana. Sina maana kwamba kwa sasa hivi siyo bora, isipokuwa wote ambao tulikuwa tunacheza nafasi za mbele tulikuwa na uwezo wa kufunga mabao. Ndio maana ulikuwa msimu ambao timu ilifunga mabao mengi (62).”
Ukiachana na ushindani wa namba aliyekuwa anakimbizana kufunga na Kagere alikuwa Salum Aiyee akiwa Mwadui aliyemaliza nafasi ya pili kwa mabao 18 akifuatiwa na Heritier Makambo (Yanga) mabao 17, John Bocco (Simba 16), Emmanuel Okwi (Simba 15), Dickson Ambundo (Alliance 12), Donald Ngoma (Azam 11) na Eliud Ambokile (Mbeya City 10).
“Kwa asilimia kubwa kila timu ilikuwa na wafungaji wa mabao mengi ndio maana nasisitiza ushindani ulianzia kikosini hadi kwa wapinzani,” alisema.
Msimu wa 2018/19 mabao 23
2019/20 mabao 22
2020/21 mabao 16
2021/22 mabao Tisa
2022/23 mabao manane (Singida Black Stars)
2023/24 mabao mawili (Namungo)
2024/25- bao-0