Mwanza. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chonchorio anadaiwa kupotea tangu Machi 23, 2025 baada ya kutoka nyumbani akidai anakwenda kufanya mazoezi.
Akizungumza na Mwananchi Jumatatu Machi 24, 2025 nyumbani kwa kada huyo mtaa wa Temeke wilayani Nyamagana, dada yake, Monari Nyanswi amesema kaka yake hakurudi tangu siku hiyo alipotoka nyumbani kwake saa 2 asubuhi na kwenda kufanya mazoezi.
Amesema baada ya saa kadhaa kupita bila kurudi nyumbani kwake walianza kumpigia simu yake ambayo haikupatikana, hivyo kulazimika kutoa taarifa kituo cha polisi.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chonchorio anayedaiwa kupotea.
“Tumeshatoa taarifa Polisi, kwa hiyo tumeiachia Serikali ishughulikie suala hili. Tunaamini kwamba Mungu atamtetea huko alipo,”amesema.
Taarifa ya Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Audax Majaliwa imeelezea kupokea taarifa za kupotea kada huyo ambaye pia ni mfanyabiashara.
“Jeshi limeanza kufanya uchunguzi, hata hivyo mpaka sasa hajapatikana.
“Ilipofika saa 5:00 asubuhi ndugu Daniel Chonchorio Nyamhanga, hakurejea nyumbani hali iliyoifanya familia yake kuingiwa na wasiwasi, hivyo kulazimika kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi.
“Taarifa hizo zilipokelewa na uchunguzi kuanza mara moja, huku Jeshi la Polisi likishirikiana kwa karibu na familia, ndugu, jamaa na marafiki. Hata hivyo ndugu Daniel Chonchorio Nyamhanga, hadi sasa hajapatikana,”ilieleza taarifa hiyo.

Dada wa Daniel, Monari Nyanswi akizungumzia tukio la kaka yake kupotea.
Taarifa hiyo pia imesema kada huyo ana makazi mengine Tarime Rorya Mkoa wa Mara na Dar es Salaam, huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
“Uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea kufanyika na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza linawaomba wananchi au mtu yeyote atakayekuwa na taarifa kumuhusu Daniel Chonchorio Nyamhanga, azitoe kwenye kituo cha Polisi kilicho karibu naye au kwenye mamlaka nyingine za Serikali,”imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara, Patrick Chandi amesema hana taarifa zozote kuhusiana na kupotea kwa kada huyo ambaye anadaiwa kutangaza nia ya kugombea ubunge Tarime Mjini.