Kabla ya wito wa Trump-Putin, mashambulizi kati ya Ukraine na Urusi yasababisha majeruhi kadhaa

Ukraine na Urusi zimekuwa zikishambuliana kwa makumi ya ndege zisizo na rubani tangu Jumatatu, Machi 17, siku moja kabla ya mazungumzo ya simu yaliyotarajiwa kati ya Vladimir Putin na Donald Trump. Watu sita wamejeruhiwa kwenye ardhi ya Urusi, huku vifusi vya ndege zisizo na rubani vikianguka kwenye uwanja wa shule kwenye ardhi ya Urusi, kulingana na viongozi wa eneo hilo. Ukraine pia imeitaka Urusi kukubali kusitisha mapigano “bila masharti.”

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mashambulio mapya yamekumba pande zote mbili usiku wa Jumatatu kuamkia Jumanne, Machi 18. Mashambulizi hayo yanakuja saa chache kabla ya mazungumzo ya simu kati ya Vladimir Putin na Donald Trump, wakati ambapo uwezekano wa kusitisha mapigano nchini Ukraine unatarajiwa kujadiliwa. Ukraine, ambayo imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi ya kila siku ya Urusi kwa miaka mitatu, imejibu kwa kurusha ndege zisizo na rubani mara kwa mara katika ardhi ya Urusi.

Mashambulizi 137 ya ndege zisizo na rubani za Urusi katika usiku mmoja

Siku ya Jumatatu usiku, jeshi la Ukraine liliripoti kulengwa na ndege zisizo na rubani 137 za Urusi. Mfumo wa ulinzi wa anga uliripotiwa kuharibu ndege zisizo na rubani 63 kati ya hizo, huku 64 zikitoweka bila kusababisha uharibifu, kulingana na Jeshi la anga la Ukraine. Huko Kyiv, ndege isiyo na rubani ya Urusi ilianguka kwenye ua wa shule katika wilaya ya Desniansky, nje kidogo ya mashariki mwa mji mkuu, na kusababisha moto. Hakuna hasara iliyotokea upande wa wanafunzi, mkuu wa utawala wa kijeshi wa jiji hilo amesema kwenye Telegram.

Mashambulizi ya Urusi pia yamepiga eneo muhimu la miundombinu katika eneo la kusini mwa Zaporizhzhia siku ya Jumatatu jioni, na kusababisha zaidi ya nyumba 3,000 na vijiji vitatu kukosa umeme, kulingana na gavana wa eneo hilo. Huko Dnipropetrovsk (katikati-mashariki), shambulio lingine la ndege zisizo na rubani za Urusi “liliharibu eneo la miundombinu” Jumatatu jioni, na kusababisha “moto mkubwa,” kulingana na Sergiy Lysak, gavana wa eneo hilo.

Watu sita wajeruhiwa nchini Urusi

Kwa upande wake, Wizara ya Ulinzi ya Urusi imetangaza kuwa imedondosa ndege zisizo na rubani 46 za Ukraine katika mikoa kadhaa ya nchi. Mikoa ya mpaka ya Belgorod, Bryansk na Kursk, pamoja na eneo la Orel, imelengwa hasa.

Huko Belgorod, mwanamume mmoja alijeruhiwa vibaya na vifusi vya ndege isiyo na rubani iliyoanguka na yuko katika uangalizi mahututi, kulingana na Gavana Vyacheslav Gladkov. Raia wengine watano walijeruhiwa katika eneo la Kursk, aliongeza kaimu gavana Alexander Khinstein.

Kyiv inashinikiza Moscow kukubali kusitishwa kwa mapigano

Baada ya usiku wa ghasia zinazozidi kuongezeka, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiga aliitaka Urusi siku ya Jumanne kukubali usitishaji mapigano “bila masharti”, saa chache kabla ya Vladimir Putin na Donald Trump kukutana na kutoa wito wa kusitishwa kwa mapigano baada ya miaka mitatu ya uvamizi wa Urusi.

“Ukraine imeunga mkono pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano kwa muda wa siku 30. “Tunatarajia Urusi itakubali pendekezo hili bila masharti,” Bw. Sybiga amesema katika taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Ukraine. “Ni wakati wa (Urusi) kuonyesha kama kweli inataka amani,” ameongeza.

Mpango wa Marekani, ambao unalenga kusitisha mapigano kwa muda, unaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea kukomesha mapigano, lakini bado unategemea nia ya Moscow.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *