Kabila aondolewa kinga ya kutoshtakiwa, kufunguliwa mashitaka ya uhaini

Kabila aondolewa kinga ya kutoshtakiwa, kufunguliwa mashitaka ya uhaini

Kinshasa, DRC. Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Joseph Kabila, sasa anakabiliwa na hatari ya kufikishwa mahakamani baada ya seneti ya nchi hiyo kupitisha azimio la kumuondolea kinga ya kushitakiwa.

Katika kikao kilichofanyika jana Alhamisi Mei 22, 2025, jumla ya maseneta 88 walipiga kura ya kumuondolea kinga hiyo, huku watano wakipinga na kura tatu zikibatilishwa.

Hatua hiyo inamfungulia njia Kabila kufunguliwa mashitaka yakiwemo ya uhaini, uhalifu wa kivita, na madai ya kuunga mkono waasi wa M23 walioteka maeneo ya Mashariki mwa DRC mwaka huu.

Joseph Kabila wakati anaapishwa kuwa Rais wa DR Congo mwaka 2001.

Kabila, ambaye ni seneta kwa mujibu wa katiba ya DRC baada ya kuondoka madarakani mwaka 2019, hakufika mbele ya Seneti kujitetea kabla ya kufanyika kikao cha jana.

Inaripotiwa kwamba aliondoka nchini humo tangu mwaka 2023, jambo lililozua maswali kuhusu mahali alipo na sababu za kutohudhuria vikao vya Bunge.

Mashtaka dhidi yake yanamhusisha moja kwa moja na uasi wa kundi la M23, ambalo linatuhumiwa kutekeleza ukatili mkubwa ikiwemo mauaji, ubakaji na utekaji wa raia katika maeneo ya Kivu Kaskazini.

Serikali ya Rais Félix Tshisekedi imekuwa ikilaumu mara kwa mara viongozi wa zamani kwa kile inachokitaja kuwa ni chanzo cha migogoro ya muda mrefu Mashariki mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, wakati hayo yakiendelea mwishoni mwa mwezi Aprili, Serikali ya DR Congo ilipiga marufuku shughuli zote za chama cha kisiasa cha rais wa zamani, Joseph Kabila cha People’s Party for Reconstruction and Democracy (PPRD).

Pia, ilitangaza kutaifaisha mali zote za Kabila kwa kile kilichoelezwa kuwa na msimamo usioeleweka kwa rais huyo wa zamani wa nchi hiyo ambaye alikuwa uhamishoni.

Kabila alikuwa akiishi uhamishoni tangu alipoondoka 2023 kabla ya kurejea Aprili 18, mwaka huu.

Mwanasiasa na ofisa wa kijeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Joseph Kabila ambaye alihudumu kama Rais wa nchi hiyo kutoka Januari 2001 hadi Januari 2019.

Kiongozi huyo ilidaiwa kurejea nchini humo kupitia mpaka wa Goma, jiji ambalo waasi wa M23 walilitwaa Januari, 2025 wakati wa mapigano kati yao na jeshi la serikali.

Baada ya kurejea nchini humo, inaelezwa kuwa kiongozi huyo alionyesha nia ya kusaidia kumaliza mgogoro unaoendelea baina ya Serikali na M23.

Aprili 19, 2025 Wizara ya Mambo ya Ndani ya DRC ilitoa taarifa ikikosoa uamuzi wa Kabila kurejea nchini humo kupitia Jiji la Goma linalodhibitiwa na M23.

“Wizara inauarifu umma kuwa shughuli zote za PPRD zimesitishwa katika eneo lote la taifa,” ilisema taarifa hiyo ya wizara.

Katika taarifa nyingine, Wizara ya Sheria ya DRC ilitangaza kuwa imeamriwa kukamata mali zote zinazohamishika na zisizohamishika za Kabila.

“Hatua za kuzuia kusafiri zimechukuliwa dhidi ya washirika wake wote wanaohusika na kesi hii ya usaliti dhidi ya taifa,” ilisema wizara hiyo.

Kulingana na taarifa hizo mbili, waendesha mashitaka wameagizwa kuanzisha mashitaka dhidi ya Kabila kwa ushiriki wake wa moja kwa moja katika uasi kupitia kundi la kigaidi la AFC/M23.

Katiba ya DRC inasemaje

Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), makosa ya uhaini na uhalifu wa kivita yanachukuliwa kuwa makosa mazito na yanaweza kuadhibiwa kwa adhabu ya kifo.

Katiba ya DRC inatambua uhaini kama kosa kubwa. Kwa mfano, kuanzisha chama kimoja cha siasa katika sehemu au eneo lote la taifa kunachukuliwa kuwa uhaini na adhabu yake haifutwi na muda yaani (hakuna ukomo wa muda wa kufunguliwa mashitaka).

Uhalifu wa Kivita

Sheria ya DRC pia inatambua uhalifu wa kivita kama kosa linalotakiwa kutolewa adhabu kali. Katika marekebisho ya sheria ya mwaka 2015, uhalifu wa kivita ulijumuishwa katika Sheria ya Kanuni ya Adhabu, na hakuna ukomo wa muda wa kufunguliwa mashitaka kwa makosa hayo.

Adhabu ya kifo

Mnamo Machi 2024, Serikali ya DRC iliondoa marufuku iliyodumu miaka 20 kutotekeleza adhabu ya kifo. Tangu wakati huo, adhabu ya kifo imeanza kutekelezwa kwa makosa kama uhaini, uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya ubinadamu, ujasusi, uasi, na njama za jinai.

Kwa hivyo, mtu yeyote anayepatikana na hatia ya uhaini au uhalifu wa kivita nchini DRC anaweza kuhukumiwa adhabu ya kifo na hakuna ukomo wa muda wa kufunguliwa mashitaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *