Dar es Salaam.Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limefanya bonanza kwa timu teule za michezo ya mpira wa kikapu (Basketball) na mikono (Handball) ili kukabiliana na changamoto zinazowakumba wanamichezo.
Bonanza hilo lililenga kuimarisha afya kwa njia ya michezo, malezi ya nidhamu, usawa wa kijinsia, utashi wa kijumuiya na kupambana na changamoto za kimichezo za miaka hii zinazowakumba wanamichezo wote kwa ujumla.

Amesema hayo Mei 7, 2025 Mratibu na Rais wa Kamati ya Ufundi ya Basketball Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM), Meja Mohamed Kasui na kuongeza kuwa bonanza hilo limefanyika Mei 6, 2025 katika viwanja vya Shirika la Mizinga, mkoani Morogoro ili kuimarisha afya, mshikamano na nidhamu kwa wanamichezo wa kijeshi.
Amesema kaulimbiu ya bonanza ilikuwa “Afya, Nidhamu na Ushirikiano Kupitia Michezo.”
“Tumeamua kuandaa bonanza hili ili kupambana na changamoto za kimichezo za miaka hii zinazowakumba wanamichezo wote kwa ujumla kama vile matumizi ya mihadarati, ukosefu wa mshikamano miongoni kwa wadau wa michezo,” amesema Meja Kasui.

Pia, amegusia uhaba wa miundombinu ya kisasa, maswala ya afya ya akili kwenye michezo kama vile matumzi mihadarati, ukosefu wa mshikamano kwa wadau wa michezo pamoja na maswala ya afya ya akili kwenye michezo.
Meja Kasui amezungumzia kuhusu upangaji wa matokeo katika michezo, rushwa kubashiri kiharamu(illigal betting) na uwajibikaji wa kisheria.
Aidha, Meja Kasui amesema bonanza hilo limehusisha jumla ya washirika zaidi ya 200, wakiwemo wanamichezo kutoka timu za JKT, Ngome, Jeshi Stars, Morogoro Warriors, pamoja na timu ya wastaafu (veterans), waamuzi na viongozi wa michezo.

Naye, Mlezi na mgeni rasmi wa timu na bonanza hilo Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy amesema bonanza hilo ni nafasi ya kipekee kwa wanamichezo wa kijeshi kushiriki, kujifunza, kuburudika nankuhamasika kwa maandalizi ya mashindano yajayo ya kitaifa na kimataifa.
“Kauli mbiu ina weka umimara ikiwa na maana afya hupatikana kwa mazoezi, nidhamu ndio moyo wa Jeshi na Ushirikiano ikiwa ni nguzo ya ushindi uwanjani na hata uwanja wa medani,”amesema Jenerali Mkeremy.
Michezo iliyochezwa katika bonanza hilo ni mechi za mtoano za Basketball na Handball (wanaume na wanawake), mashindano ya 3-0n-3 Basketball na 5-0n-5 Handbali, Cross-sports (wanabasketball kucheza handbali na kinyume chake), mechi ya wastaafu (veterans) na walimu pamoja na mashindano ya ubunifu.