Jux sio wa kwanza ‘kuvuka boda’ kisa penzi 

Dar es  Salaam. Hivi karibuni Jux alifunga ndoa na mpenzi wake kutokea Nigeria, Priscilla ukiwa ni mwendelezo wa mastaa Bongo kuvuka mipaka na kwenda nchi nyingine na hata mabara ya mbali kwa lengo la kusaka mapenzi tu!. 

Wawili hao ambao waliweka wazi kwa umma uhusiano hapo Julai 2024, walifunga ndoa Dar es Salaam na kuhudhuria na ndugu wa pande zote mbili pamoja na mastaa wa Bongofleva akiwemo Diamond Platnumz na mpenzi wake Zuchu. 

Ni ndoa inayotazamiwa kuwa na mvuto wa aina yake kutokana umaarufu wa chapa zao, Jux akiwa ametamba katika muziki kwa miaka zaidi ya 10, huku Priscilla, binti wa muigizaji wa Nollywood, Ojo akifanya shughuli za mitindo na uigizaji. 

Na hii ni orodha fupi ya mastaa wa muziki Bongo wenye ndoa, uhusiano au walishakuwa nao na wenzao kutokea mataifa mengine kama alivyofanya Jux, mwanachama wa zamani wa kundi la Wakacha. 

Alikiba > Kenya

Staa huyu wa Kings Music na Rais wa Crown Media alisafiri hadi Kenya na kukutana na binti kutokea Mombasa, Aminah ambaye walifunga ndoa Aprili 2018 na kufuatiwa na sherehe kubwa pale Serena Hotel na hadi sasa wamejaliwa kupata watato wawili. 

                     

Harmonize > Italia 

Muda mfupi baada ya kuachana na WCB Wasafi, Harmonize na alimuoa mpenzi wake wa siku nyingi Sarah Michelotti kutokea Italia, ndoa hiyo ilifungwa Dar es Salaam hapo Septemba 2018 na kufikia Desemba 2019 wakaweka wazi kuachana huku wakitaja sababu. 

                     

Lady Jaydee > Nigeria

Baada ya kupata talaka kutoka kwa aliyekuwa mume wake Gardner G. Habash hapo Desemba 2016, Lady Jaydee aliingia katika uhusiano na mwanamuzi mwenzake kutokea Nigeria, Spicy ambaye wameshirikiana katika wimbo wao, Together Remix (2018). 

                     

AY > Rwanda 

Aliyekuwa mwanachama wa kundi la East Coast Team, AY mwenye albamu zake tatu sokoni, Raha Kamili (2003), Hisia Zangu (2005) Habari Ndio Hiyo (2008), alifunga ndoa hapo Februari 2018 na mchumba wake kutokea Rwanda, Remy na tayari wana mtoto mmoja. 

Rama Dee > Australia

Mshindi huyu wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2013 kama Msanii Bora wa RnB, ameoa mwanamke kutokea Australia ambaye tayari wamejaliwa watoto, huko Rama Dee akihamia nchini humo na kununua nyumba na kuendelea na shughuli zake. 

Vanessa Mdee > Marekani

Kwa sasa anaishi huko Georgia, Marekani na mpenzi wake Rotimi mwenye asili ya Nigeria ambaye alimvisha pete ya uchumba Desemba 2020 na tayari wana watoto wawili, huku Vanessa akitokea katika video ya wimbo wa Rotimi, Love Somenody (2020). 

                     

Ben Poul > Kenya 

Mwimbaji huyo wa RnB alifunga ndoa na Anerlisa kutokea Kenya Mei 2020 ila baada ya mwaka mmoja wakaripotiwa kuachana ingawa talaka rami ilikuja kutoka Septemba 2021 ikiwa ni baadaye mrembo huyo kuonekana katika video ya Ben Pol, Kidani (2020). 

Chindoman > Marekani

Anatokea kundi la Watengwa lenye maskani Arusha, kwa sasa anaishi Los Angeles, California nchini Marekani na ameoa huko na tayari yeye na mkewe wamejaliwa kupata watoto huku akiendelea na harakati zake za muziki wa Hip Hop uliomtambulisha. 

Diamond > Uganda & Kenya 

Mwanzilishi huyu wa WCB Wasafi alikuwa na uhusiano na Zari The Bosslady kutokea Uganda na wakaachana 2018 wakiwa na watoto wawili. Kisha akaja kuwa na Tanasha Donna wa Kenya ambaye walishirikiana katika wimbo, Gere (2020) huku wakipata mtoto mmoja.