Dar es Salaam. Wakiwa na miezi sita tangu kuweka wazi uhusiano wao, Jux na Priscilla Ojo ‘Hadiza’ wamekuwa wakitoa somo zuri kwa mashabiki na wadau wa Bongo kuhusiana na maana ya mahusiano.
Achana na ile ya Nandy na Billnass, au ya Aika na Nahreel ukiwakutanisha wote unaweza kusema vipo vitu vya kujifunza kutoka kwa wawili hao ambao wameiteka mitandao ya kijamii kutokana na mapenzi yao.

Uhusiano wao unadaiwa kuanza mwishoni mwa mwaka 2023 lakini waliuweka wazi Agosti 2024 huku mambo yakishamiri zaidi baada ya Jux kwenda ukweni Nigeria ambapo alipokelewa kwa shangwe na mkwe wake ambaye ni mwigizaji mkongwe Nigeria Iyabo Ojo.
Hatimaye, Februari 7, 2025, wawili hao walithibitisha mapenzi yao kuwa ya kweli ambapo walifunga ndoa ya Kiislamu. Ikawa moja ya harusi kubwa zilizovuta hisia za mashabiki kutoka Tanzania, Nigeria, na kwingine.

Japo kumekuwa na komenti baadhi katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa ‘Wataachana Tuu’ lakini wawili hao wameendelea kuwakera watesi wao. Ambapo usiku wa kuamkia leo Februari 13, 2025, Jux alifanikiwa kumvisha pete ya pili mpenzi wake huyo mbele ya familia yake.
“Baby, nakuchumbia kwa mara ya pili, lakini safari hii mbele ya familia yako na marafiki zako wa karibu, na pete yenye ukubwa mara mbili, Nakupenda kwa moyo wangu wote, na siwezi kusubiri kutumia maisha yangu yote pamoja na wewe, mpenzi wangu,” ameandika Jux katika ukurasa wake wa Instagram.

Hata hivyo, ikumbukwe Jux kupata jiko Nigeria kunaweza kuwa moja ya njia ya kumpatia mashabiki wengi zaidi kimataifa ukizingatia Nigeria ndilo taifa lenye watu wengi zaidi barani Afrika.