
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani vikali kitendo cha hivi karibuni cha utawala ghasibu wa Israel cha uchokozi dhidi ya vituo kadhaa vya Iran, na kukitaja kuwa ni ukiukaji mkubwa wa mamlaka ya kujtawala ya Iran.
OIC ilitangaza katika taarifa yake siku ya Alhamisi kwamba hatua za kichokozi za utawala ghasibu wa Israel ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa, pamoja na ukiukwaji wa wazi wa mamlaka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mipaka yake.
Taarifa hiyo, iliyonukuliwa na mashirika ya habari ya Iran, inakuja wiki mbili baada ya ndege za kivita za Israel kutumia kituo cha wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kurusha makombora ya masafa marefu yaliyolenga vituo vya kijeshi katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam nchini Iran. Shambulio hilo liliwauwa maafisa wanne wa Jeshi la Iran na raia mmoja.
Mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran ulifanikiwa kuzuia na kukabiliana na uchokozi huo.
OIC pia imelaani vikali ukiukaji wa mamlaka ya Iraq uliofanywa na utawala wa Israel, huku taasisi hiyo ikitumia anga ya nchi hiyo ya Kiarabu kutekeleza kitendo cha uchokozi dhidi ya Iran.
OIC imesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi nyingine zilizoathirika zinahifadhi haki ya kimsingi kulinda mamlaka yao, mipaka na usalama na raia kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
OIC imesisitiza kwamba ukatili unaoendelea wa Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, hususan huko Gaza, Lebanon, pamoja na vitendo vyake vyenye nia mbaya katika maeneo mengine ya Asia Magharibi vinatishia amani, usalama na utulivu wa eneo hilo.
Kwa kumalizia OIC imetoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama chombo kikuu kinachohusika na kudumisha amani na usalama wa kimataifa kuchukua hatua za haraka za kuzuia uchokozi wa utawala katili wa Isarel.
Maafisa wa Iran wamesema Jamhuri ya Kiislamu itajibu uchokozi huo wa hivi wa Israel na kwamba haitaacha haki yake ya kujilinda.