
Jumuiya ya kimataifa imeitaka Rwanda kuondoa wanajeshi wake nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na kuacha kuwafadhili waasi wa M23 wanaosema kwamba wanalenga kusonga mbele hadi mji mkuu, Kinshasa.
Kwa mujibu wa DW, shinikizo hilo linaongezeka kwa utawala wa Rais Paul Kagame wakati waasi wa M23 wakiendelea kusonga mbele kuelekea mji mwengine wa Mashariki mwa Congo, Bukavu.
Mapigano yameendelea kuripotiwa maeneo mbalimbali mashariki mwa DRC ambapo waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wakielekea katika mji wa Bukavu baada ya kuchukua udhibiti kamili wa Goma.
Licha ya mapigano kupungua huko Goma, hali ya kibinadamu inaelezwa kuwa mbaya. Uhaba wa chakula na bidhaa muhimu, mgawo wa umeme umevurugika, hakuna maji safi huku kukiwa matatizo pia kwenye mtandao wa intaneti.
Raia wa Goma wamesema wanahitaji msaada kwa kuwa mji wao umekuwa kama meli isiyo na nahodha. Hawa ni Isaac Mastaki na Louise Furaha.
Hayo yanajiri wakati kiongozi wa kisiasa wa muungano wa waasi wa Kongo unaolijumuisha kundi la M23 Corneille Nangaa ameapa hapo jana kuwa wapiganaji wake hawatauachia mji wa Goma na kusema wataendelea kusonga mbele zaidi ndani ya ardhi ya Kongo hadi mji mkuu Kinshasa. Hata hivyo bwana Nangaa alisema wako tayari kwa mazungumzo na serikali ya Kongo.
Rais wa DRC, Felix Tshisekedi alitoa wito wa kufanyika kwa uhamasishaji mkubwa wa kijeshi ili kukabiliana na uasi huo huku akitupilia mbali miito ya kufanya mazungumzo na waasi wa M23.
Katika ujumbe wa video, Waziri wa Ulinzi wa DRC, Guy Kabombo Muadiamvita amesema hakuna mpango wowote unaowezekana wa mazungumzo na M23 akisema watasalia Congo na kupambana hadi kifo.
Juhudi za kikanda na kimataifa zinaendelea ili kuutafutia suluhu mzozo huo. Rais Kagame wa Rwanda na Tshisekedi wa DRC walizungumza na Rais wa Angola Joao Lourenco ambaye aliteuliwa na Umoja wa Afrika kuwa mpatanishi katika mzozo huo, na wote wawili waliafiki kutoa ushirikiano wao.
Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noel Barrot aliwasili nchini Rwanda jana na kukutana na Rais Kagame baada ya kufanya mazungumzo na Rais Tshisekedi mjini Kinshasa.
Alipoulizwa kuhusu kinachoendelea huko DRC, Rais wa Marekani, Donald Trump alisema mzozo kati ya DRC na Rwanda ni tatizo kubwa lakini akakataa kutoa maoni yake zaidi.
Mzozo huo unaweza kuikosesha Rwanda misaada ya mamilioni ya dola kutoka kwa washirika wake wa Magharibi baada ya kuonekana kukaidi miito ya kuondoa wanajeshi wake huko DRC na kuacha kuwaunga mkono waasi wa M23.
Serikali ya Uingereza imesema inatarajia kutathmini upya msaada wake kwa Rwanda kutokana na kuhusika kwake katika mzozo wa mashariki mwa DRC.
Jumanne iliyopita, Ujerumani ilisitisha mkutano uliopangwa kufanyika na maofisa wa Rwanda mwezi ujao na kusema inajadiliana na wafadhili wengine wa kimataifa kuhusu hatua zaidi zinazoweza kuchukuliwa.
Rwanda iwekewe vikwazo
Wakati huohuo, Serikali ya DRC imetoa wito wa Rwanda kuwekewa vikwazo na kupunguzwa kwa misaada inayopelekewa na pia isimamishwe ushiriki wake katika misheni ya kulinda amani ya UN kwa jukumu ambalo inadaiwa kutekeleza katika mzozo wa Mashariki ya Congo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC, Therese Kayikwamba Wagner amenukuliwa na BBC akisema Rwanda inakalia eneo la nchi yake kinyume cha sheria.
Alisema Rwanda inaunga mkono, kufadhili na kuandaa ujasusi ambao unatafuta kupindua serikali iliyochaguliwa kisheria.
Akijibu madai hayo, Msemaji wa Serikali ya Rwanda amesema nchi yake inatetea mipaka yake wala haina nia ya kubadilisha serikali. Amesema Rwanda ilikuwa imepeleka mifumo ya kujihami kuzuia kusambaa kwa mapigano kutoka Congo hadi nchini humo.
Vikosi vya RDF mpakani
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo ameiambia BBC kwamba nchi yake imepeleka vikosi vyake katika maeneo ya kujihami na mashambulizi ili kuepuka kusambaa kwa mzozo huo mashariki mwa DRC.
Hayo yanajiri wakati Serikali ya DRC ikitaka jumuiya ya kimataifa kuiwekea vikwazo dhidi ya Rwanda, ambayo wanaituhumu kupeleka wanajeshi katika ardhi yake kwa ajili ya kuwaunga mkono waasi wa M23 waliouteka mji muhimu wiki hii.
Shinikizo la kimataifa linaongezeka kwa Rwanda kuondoa wanajeshi wake mashariki mwa DRC.
Licha ya ushahidi unaoongezeka kwamba wanajeshi wake wanapelekwa kusaidia na kuongoza mashambulizi ya waasi wa M23, serikali mjini Kigali inasisitiza kuwa inadumisha tu usalama wake wa eneo hilo kwenye mpaka.
Makolo amesema watu wasiopungua 15 wameuawa Rwanda kwa makombora kutoka DRC. Alisema hatua yoyote ya mashambulizi ya Rwanda itatokea mbali na ardhi yake ambayo labda inamaanisha kuwa hatua kama hiyo ya kijeshi inaweza kutokea nchini Congo.
Lakini baadhi ya wafadhili wa Kigali kama Uingereza na Ujerumani wanachunguza upya msaada wao kwa Rwanda wakiituhumu kwa kuwaunga mkono waasi. Zaidi ya asilimia 40 ya bajeti yake ya kitaifa inafadhiliwa kupitia misaada ya kigeni.