
Jumuiya 11 zisizo za kiserikali (NGO’s) nchini Ufaransa zimeitaka serikali ya nchi hiyo itekeleze agizo la Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ya kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mkuu wa zamani wa ulinzi Yoav Gallant.
Jumuiya hizo, ikiwa ni pamoja na Human Rights League (LDH) na Chama cha Mshikamano wa Palestina cha Ufaransa (AFPS), zimetoa taarifa ambayo imeitaka Ufaransa kuifanyia kazi hati ya ICC inayoamuru kukamatwa viongozi hao wa utawala wa Kizayuni wanaotuhumiwa kuhusika na jinai za kivita.
Taarifa hiyo imesisitizia haja ya serikali ya Ufaransa kuhakikisha inawakamata maafisa hao iwapo wataingia katika ardhi ya Ufaransa.
Aidha, imeishinikiza Paris kuendelea kuiunga mkono ICC licha ya mahakama hiyo kukabiliwa na mashinikizo mbalimbali kutoka nje, ikisisitiza: “kutolewa kwa hati hizi kunasisitizia zaidi haja ya kuziwekea vikwazo mamlaka za Israel.”
Waziri Mkuu wa zamani wa Ufaransa Dominique de Villepin, ameuzungumzia waranti wa ICC kwenye televisheni ya LCI ya nchi hiyo; na alipoulizwa kama Ufaransa inapaswa kutekeleza uamuzi huo ikiwa Netanyahu ataingia kwenye ardhi ya Ufaransa au Ulaya, de Villepin alijibu: “Ufaransa tayari imejibu suali hili kupitia Waziri wa Mambo ya Nje wa zamani Stephane Sejourne, akisema, ‘Bila shaka, Ufaransa itatekeleza uamuzi wa ICC.”
Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, ICC siku ya Alkhamisi ilitangaza kwamba imetoa hati za kukamatwa Netanyahu na Gallant, kwa kuhusika na “jinai za kivita na jinai dhidi ya ubinadamu uliofanywa huko Ghaza.”
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa Christophe Lemoine, alikwepa kujibu moja kwa moja kama Ufaransa itatekeleza vibali hivyo, wakati wa mkutano wa kila wiki na wanahabari aliposema, hilo ni “suali tata kisheria”…/