Jumatatu tarehe 14 Oktoba 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Mfunguo Sita Rabiuthani 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Oktoba 2024.

Miaka 1245 iliyopita inayosadifiana na tarehe 10 Rabiuthani mwaka 201 Hijria, alifariki dunia Bibi Fatima Maasuma A.S, binti wa Imam Mussa bin Ja’far al-Kadhim (as).

Bibi Fatima Maasuma alizaliwa mwaka 173 Hijria katika mji wa Madina. Alikuwa mwanamke mwenye fasaha katika uzungumzaji, alimu, hodari na zahidi na mcha- Mungu.

Mwaka mmoja baada ya kaka yake yaani Imam Ali bin Mussa Ridha (as) kuwasili Khurasan nchini Iran, Bibi Maasuma aliondoka Madina kwa lengo la kumfuata kaka yake, lakini akiwa njiani alisimama katika mji wa Qum na kufariki dunia mjini humo kutokana na maradhi au kwa mujibu wa kauli nyingine, kutokana na sumu aliyeopewa.   

Siku kama ya leo miaka 210 iliyopita, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulifanyika kwa lengo la kujadili  “Ulaya baada ya Napoleon Bonaparte”. 

Baada ya kujiuzulu na kubaidishwa Bonaparte mwezi Aprili mwaka 1814, mkutano wa kihistoria wa Vienna ulianza kufanyika katika siku kama ya leo katika mji mkuu wa Austria Vienna ili kuchukua maamuzi kuhusu ardhi zilizokaliwa kwa mabavu na Ufaransa katika kipindi cha vita vya Bonaparte.

Wakati wa kuendelea mkutano huo, Napoleone Bonaparte alikimbia kutoka mahala alipokuwa amebaidishiwa na mwishoni mwa mwezi Februari mwaka 1815 kwa mara nyingine tena akashika hatamu za uongozi kwa muda mfupi, kipindi ambacho kiliondokea kuwa mashuhuri kwa jina la “Utawala wa Siku 100”.

Aliposhika tena hatamu za uongozi alijianda kuwashambulia maadui zake.   

Mkutano wa Vienna

Siku kama ya leo miaka 91 iliyopita, kwa amri ya Adolf Hitler Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, nchi hiyo ilijitoa katika Jumuiya ya Kimataifa.

Kuingia madarakani Adolf Hitler akiwa Kansela wa Ujerumani kulizushha wasiwasi mkubwa katika kila kona ya Ulaya kutokana na mipango yake ya kijeshi.

Baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kutiwa saini mkataba wa amani wa Warsaw ambao ulidhibiti sana zana za kijeshi za Ujerumani, Hitler na viongozi wengine wa Kinazi walikasirishwa mno na hatua hiyo. 

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, Wazayuni wa Israel walivamia kijiji cha Qibya kilichoko katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kufanya jinai kubwa za kutisha.

Katika mashambulizi na uvamizi huo ulioendelea katika kijiji hicho kwa muda wa siku mbili, Wazayuni walitekeleza mauaji na ukatili mkubwa dhidi ya raia wa Kipalestina wasio na hatia. Mbali na Wazayuni hao kuwaua na kuwajeruhi kwa umati raia wa Kipalestina zaidi ya 42, askari wa Israel waliokuwa wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ariel Sharon, walibomoa makumi ya nyumba na shule za kijiji hicho.

Mauaji hayo ya halaiki ni miongoni mwa mifano ya ugaidi wa utawala ghasibu wa Israel hususan wa Waziri Mkuu wa zamani wa utawala huo, Ariel Sharon. 

Mauaji ya Wazayuni katika kijiji cha Qibya

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, yaani tarehe 14 Oktoba mwaka 1964 Nikita Khrushchev, Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti cha Umoja wa Sovieti aliuzuliwa kutoka katika wadhifa wake huo.

Nikita Khrushchev alifanikiwa kuwa mwanachama wa ofisi ya kisiasa ya Chama cha Kikomonisti mwaka 1939 na baada ya kufariki dunia Joseph Stalin mwaka 1953, Nikita alijitokeza kuwa shakhsia aliyekuwa na nguvu katika umoja wa Sovieti na kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti na baadaye Waziri Mkuu wa shirikisho hilo. 

Nikita Khrushchev

Na katika siku kama ya leo miaka 25 iliyopita alifariki dunia kiongozi wa zamani wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Nyerere Alizaliwa Butiama huko Mara mwaka 1922. Mwaka 1955 aliingia katika ulingo wa siasa huku akiongoza chama cha (Tanganyika Africa Nation Union) TANU. Mwaka 1961 Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Tanganyika na mwaka mmoja baadaye akawa rais wa nchi hiyo. Kutokana na juhudi zake mwaka 1964 ziliungana Tanganyika na Zanzibar na kuunda nchi moja ya Jamhuri ya Muunganio wa Tanzania.

Nyerere aliendelea kuongoza nchi hiyo hadi mwaka 1985 ambapo aliachia hatamu za uongozi. Licha ya hayo, lakini Nyerere aliendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za Tanzania hadi alipofariki dunia.