Jumatatu, 28 Oktoba, 2024

Leo ni Jumatatu tarehe 24 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 28 Oktoba 2024.

Siku kama ya leo miaka 99 iliyopita yaani tarehe 7 Aban mwaka 1305 Hijria Shamsia Ayatullah Sayyid Hassan Modarres aliyekuwa miongoni mwa wanazuoni na wanamapambano maarufu nchini Iran alinusurika jaribio la kuuawa.

Ayatullah Sayyid Hassan Modarres

Jaribio hilo lilifanywa na vibaraka wa Shah Reza Pahlavi aliyekuwa maarufu kwa udikteta, ukatili na upinzani mkubwa dhidi ya maulama wa Kiislamu. Uhasama wa utawala wa kifalme wa Pahlavi dhidi ya Ayatullah Modarres ulitokana na mchango mkubwa wa mwanazuoni huyo wa Kiislamu katika kuwaamsha wananchi na kufichua njama za utawala wa Kipahlavi na muungaji mkono wake yaani serikali ya Uingereza.

Kwa kipindi fulani Ayatullah Modarres alikuwa mwakilishi wa wananchi wa Tehran katika Bunge. Baada ya kunusurika kifo katika jaribio hilo Ayatullah Modarres alipelekwa uhamishoni kwa amri ya mfalme dikteta Reza Khan na muda mfupi baadaye aliuawa shahidi na vibaraka wa Shah.   ***

Miaka 76 iliyopita katika siku kama ya leo, wakati wa vita vya kwanza kati ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Waarabu, wanajeshi wa utawala huo waliwaua kwa umati wakazi wa kijiji cha al Dawayima huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Jinai za Wazayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu

Wazayuni hao walivamia msikiti wa kijiji hicho na kuwauwa shahidi Waislamu 75 raia wa Palestina waliokuwa wakiswali. Vilevile waliwaua kwa umati watu wa familia 35 waliokuwa wamekimbilia hifadhi katika pango moja nje ya kijiji hicho.

Askari jeshi wa utawala haramu wa Israel walikisawazisha na ardhi kijiji hicho baada ya kuwaua kwa umati wakazi wake wote. ***   ***

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, ulihitimishwa mgogoro wa makombora wa Cuba baada ya kiongozi wa wakati huo wa Urusi, Nikita Khrushchev kuamuru kurejeshwa nyumbani meli zilizokuwa na makombora ya nyuklia.

Hatua ya Urusi ya kujenga vituo kadhaa vya makombora ya nyuklia nchini Cuba katika umbali wa kilomita 90 kutoka Marekani ilizusha mgogoro mkubwa wa makombora uliokaribia kuitumbukiza dunia katika vita vya nyuklia. Wakati huo Marekani na Russia zilitishia kushambuliana kwa makombora ya nyuklia na kuzusha hofu kubwa hususan kwa watu wa Marekani, Russia na nchi za Ulaya.

Hatimaye tarehe 28 Oktoba mwaka 1962 Nikita Khrushchev alitoa amri ya kurejea nchini meli zote zilizokuwa na makombora ya nyuklia na kufungwa vituo vya makombora vya Urusi nchini Cuba. ***   

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, alifariki dunia Taha Hussein mwandishi mahiri na stadi wa Kimisri.

Alizaliwa mwaka 1889 katika moja ya vijiji vya Misri. Taha Hussein ambaye alikuwa mtoto wa saba katika familia yake, alipofuka na kupoteza uwezo wa kuona akiwa na umri wa miaka mitatu. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimjaalia kipaji cha hali ya juu. Taha Hussein alifanikiwa kuhafidhi Qur’ani yote katika kipindi kifupi.

Chuo Kikuu cha al-Azhar

Akiwa na umri wa miaka 14 alifaulu mtihani wa watahaniwa wa kuingia Chuo Kikuu cha al-Azhar na akiwa pamoja na kaka yake, alijishughulisha na kusoma masomo ya dini pamoja na lugha ya kigeni. Mwaka 1914 Taha Hussein alihitimu kwa alama nzuri na kutunukiwa shahada ya uzamivu yaani PhD. Wakati huo Chuo Kikuu cha Taifa cha Misri kilichukua uamuzi wa kuipeleka timu ya wahadhiri nchini Ufaransa kwa ajili ya kufundisha historia ya Mashariki. Akiwa ahuko alijifunza histotia ya Ugiriki na Roma ya kale pamoja na lugha ya Kigiriki.

Mwaka 1959 mwandishi huyo mahiri wa Kimsri alinutukiwa tuzo ya Nobel kutokana na mchango wake katika uga wa fasihi. Taha Husserin ameandika vitabu vingi katika taaluma za fasihi, sayansi ya siasa na historia. ***