Leo ni Jumapili 15 Mfunguo Nane Jamad al-Awwal 1446 Hijria mwafaka na 17 Novemba 2024 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1408 iliyopita, Muhammad Abuu Bakr mmoja wa masahaba watiifu wa Imamu Ali (as) na kamanda mashuhuri wa Kiislamu aliuawa shahidi katika vita na wanajeshi wa Amr bin al-As. Muhammad Abu Bakr ambaye alikuwa ameteuliwa na Imamu Ali kuwa mtawala wa Misri alikabiliwa na uasi tofauti tofauti. Muawiya mtawala wa Bani Umayyah akitumia vibaya mazingira hayo alimtuma Amr bin As huko Misri akiwa pamoja na wanajeshi 6,000. Muhammad bin Abu Bakr akiwa na wanajeshi 2000 alishindwa kkatika vita hivyo. Baada ya kutiwa mbaroni aliunguzwa katika moto na kufa shahidi.

Siku kama ya leo miaka 307 iliyopita, Jean le Rond d’Alembert mwanahisabati wa Kifaransa alizaliwa katika mji wa Paris huko Ufaransa. Baba na mama yake walimtelekeza kando ya kanisa moja mjini Paris akiwa mtoto mchanga. Aliokotwa na kulelewa na mwanamke na mwanaume mmoja waliokuwa wauza vioo. Jean le Rond d’Alembert alisoma kwa bidii na baada ya kuhitimu masomo ya kati alianza kusoma taaluma ya tiba na sheria. Hata hivyo baada ya muda aliondokea kuipenda mno taaluma ya hisabati ambapo alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo. Alipotimiza umri wa miaka 22 d’Alembert alizindua makala kuhusiana na hesabu, makala ambayo yalimpatia umashuhuri mkubwa. Ameacha athari mbalimbali ambazo zipo katika maktaba za Ufaransa. Jean le Rond d’Alembert alifariki dunia tarehe 29 Oktoba 1783 akiwa na umri wa miaka 66.

Siku kama ya leo miaka 228 iliyopita, Catherine The Great malkia mashuhuri wa Russia aliaga dunia. Alizaliwa Mei Pili 1729 na akiwa na umri wa miaka 15 aliolewa na Peter III. Hata hivyo Peter III mfalme wa wakati huo wa Russia hakuwa akimpenda mkewe huyo na alikuwa akimvunjia heshima na kumdhalilisha mbele za watu. Mwaka 1762 wakati Peter III alipokuwa ametoka nje ya mji, Catherine the Great alijitangaza kuwa malkia wa Russia. Peter III ambaye alishtushwa na kupata pigo kwa hatua hiyo alilazimika kujiuzulu pasina ya mapambano na baada ya siku chache akaaga dunia.

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, Robert Owen mpigania mageuzi ya kisoshalisti wa Wales na mmoja wa waasisi wa Harakati ya Usoshalisti aliaga dunia. Alianza harakati zake tangu akiwa na umri wa miaka 18 sambamba na kujenga kiwanda cha ufumaji. Katika kiwanda chake hicho kwa mara ya kwanza alianza kuboresha hali ya afya na ustawi wa wafanyakazi barani Ulaya kwa kupunguza masaa ya kazi kutoka masaa 14 kufikia masaa 10.

Katika siku kama ya leo miaka 155 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 17 Novemba mwaka 1869, Mfereji wa Suez unaounganisha Bahari ya Mediterania na Bahari Nyekundu ulifunguliwa. Uchimbaji wa mfereji huo ulisimamiwa na mhandisi wa Kifaransa Ferdinand de Lesseps katika kipindi cha miaka 10 huku ukiwa na urefu wa kilomita 168 na upana wa mita 120 hadi 200. Karne kadhaa kabla yake, Mfalme Daryush wa Iran na baadhi ya wafalme wa Misri walichukua hatua kadhaa za kuanzisha mfereji baina ya bahari hizo mbili, suala ambalo linaonyesha umuhimu wa Mfereji wa Suez unaopunguza kwa kiasi kikubwa masafa ya kutoka Asia kuelekea Ulaya, safari ambayo zamani ilikuwa ikifanyika kupitia Afrika Kusini.
