Leo ni Jumapili 8 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na 10 Novemba 2024 Miladia.
Miaka 541 iliyopita muwafaka na leo, alizaliwa Martin Luther, mpigania mageuzi ya kidini wa Kijerumani. Luther alikuwa padri wakati akiwa kijana. Mitazamo ya Martin Luther kuhusiana na dini ya Kikristo ilitofautiana na baadhi ya mitazamo ya Papa na viongozi wa ngazi ya juu wa Kanisa na kuanzia mwaka 1517, Luther alidhihirisha mapambano na upinzani wake dhidi ya dhulma na ukandamizaji wa Kanisa Katoliki. Martin Luther alipinga waziwazi agizo la Papa wa Kanisa Katoliki na akaifasiri Injili kwa lugha ya Kijerumani. Baada ya hapo aliaanzisha harakati ya kiprotestanti dhidi ya kanisa hilo.
Siku kama ya leo miaka 225 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba mwaka 1899, kulitokea mapinduzi ya kijeshi yaliyofahamika kwa jina la Brumaire nchini Ufaransa. Brumaire lilikuwa jina la mwezi wa pili katika kalenda ya mapinduzi ya Ufaransa ambao unaenda sambamba na mwezi wa Novemba kwa kalenda ya Milaadia. Siku hiyo Napolione Luis Banaparte ambaye alikuwa katika jitihada a kuteka na kukalia nchi za kaskazini mwa Afrika, alirejea kwa siri nchini Ufaransa kufuatia mwaliko wa kiongozi mmoja wa utawala wa nchi hiyo. Luis Banaparte alifanikiwa kupindua utawala uliokuwepo nchini Ufaransa kwa kutegemea uungaji mkono wa askari jeshi na Bunge la nchi hiyo na kuanza kuiongoza rasmi Ufaransa.

Siku kama ya leo miaka 135 iliyopita, alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 68 Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini, mtaalamu wa sheria za Kiislamu (fiqhi), mtafiti na mtaalamu wa Hadithi wa Kishia. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alielekea Qazvin na baada ya hapo alielekea Isfahan kwa ajili ya masomo ya juu. Baada ya kustafidi na maulama wakubwa wa mji wa Isfahan alifanya ziara katika maeneo matakatifu nchini Iraq ambapo alikaa miaka kadhaa akijiendeleza kimasomo. Alirejea Qazvin na kuanza kazi ya ufundishaji na kutoa fatwa. Ayatullah Mullah Ahmad Khoeiini Qazvini ameacha athari kadhaa kama vile ‘Mi’raajul-Wusuuli ila ilmil-Usuul’ chenye juzuu mbili, ‘Lawaamiu fil-Fiqhi’ chenye juzuu tatu na ‘Mir-atul-Muraadi fi Ilmir-Rijaal.’ ***

Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita aliaga dunia Sheikh Muhammad Abduh ambaye alikuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika mji wa Alexandria nchini Misri. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha al Azhar na kisha akahudhuria darsa za Jamaluddin Asadabadi, mwanazuoni aliyepigania uhuru wa nchi za Kiislamu. Baada ya kupelekwa uhamishoni Sayyid Jamaluddin, Sheikh Muhammad Abduh alichukua nafasi yake ya kufundisha na kutoa elimu kwa wanazuoni na wanafikra za Kiislamu. Hata hivyo Sheikh Abduh alibaidishiwa nchini Syria baada ya satuwa ya wakoloni wa Kiingereza kuenea nchini Misri. Baada ya kufunza kwa kipindi cha miaka sita nchini Syria alihamia Paris na kusaidiana na Sayyid Jamaluddin Asadabadi katika kuchapisha gazeti la al Uruwatul Wuthqaa.

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita yaani tarehe 10 Novemba 1912, Morocco alianza kukoloniwa na Ufaransa na Uhispania. Kabla ya hapo nchi hiyo inayopatikana kaskazini mwa Afrika ilikuwa ikikaliwa na madola mbalimbali kama vile dola la Othmania, Roma na Italia. Baadaye Uhispania na Ufaransa zilianza kukosana, na muungano wao katika kuikoloni Morocco ukavunjika. Ufaransa iliendelea kuikoloni nchi hiyo na baada ya muda usio mrefu, wananchi wakaanzisha mapambano dhidi ya Wafaransa. Hatimaye mapambana hayo yalipata ushindi na Morocco ikajipatia uhuru 1956.

Miaka 60 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 10 Novemba 1964, Leonid Brezhnev alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomunisti cha CPSU katika Urusi ya zamani na hivyo kuchukua rasmi jukumu la kukiongoza chama hicho. Brezhnev aliendelea kushikilia cheo hicho cha ukatibu mkuu hadi kifo chake mwaka 1982. Katika kipindi chake cha uongozi, Umoja wa Kisovieti ulipata nguvu zaidi kijeshi lakini pia ulikumbwa na matatizo mengi ya kiuchumi. Viongozi wa kikomunisti waliokuja baada yake walisema matatizo aliyoyaacha Leonid Brezhnev ndiyo yaliyosababisha kuporomoka na kuvunjika kabisa Umoja wa Kisovieti mwaka 1991.

Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio nambari 3379 lililoutambua Uzayuni (Zionism) kuwa ni aina fulani ya ubaguzi wa kizazi. Azimio hilo lilitoa pigo kubwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel na kufichua utambulisho halisi wa utawala huo. Azimio hilo la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliikasirisha sana Israel na waungaji mkono wa utawala huo wa kibaguzi hususan Marekani. Tofauti na mafundisho ya Kiyahudi, fikra za Uzayuni ambazo zilianzishwa mwishoni mwa karne ya 19 zinawatambua wafuasi wa dini hiyo kuwa ni ndio kizazi bora zaidi ya wengine wote duniani. Kwa mujibu wa fikra hiyo Wazayuni wa Israel wanawatambua watu wa Palestina kuwa ni kizazi duni na hakiri zaidi na kwa sababu hiyo wanawakandamiza, kuwaua na kuwafukuza katika makazi na nchi yao.

Na tarehe 10 Novemba mwaka 1981 yaani miaka 43 iliyopita wakati wa vita vya Saddam Hussein dhidi ya Iran, Ufaransa na Iraq zilitiliana saini mkataba wa mauzo ya silaha uliokuwa na thamani ya dola bilioni moja. Mkataba huo ulikuwa moja kati ya mikataba kadhaa ya mauzo ya silaha baina ya Ufaransa na utawala wa dikteta wa zamani wa Iraq wakati wa mashambulizi ya Iraq dhidi ya Iran. Ufaransa ilikuwa bega kwa bega na utawala wa Saddam Hussein tangu mwanzoni mwa mashambulizi na uvamizi wa Iraq dhidi ya Iran na ilihesabiwa kuwa muuzaji mkubwa wa pili wa silaha kwa utawala wa dikteta Saddam Hussein baada ya Russia. Silaha hizo zilijumuisha ndege za kisasa za kivita, makombora ya aina mbalimbali, vifaru, mizinga na aina nyingine za zana za kivita. Ufaransa pia ilimsaidia Saddam Hussein katika kutengeneza silaha za kemikali. Vilevile iliupatia utawala wa Iraq mkopo wa dola bilioni 5 wakati wa vita vyake dhidi ya Iran na imekataa kulipa deni la dola bilioni moja kwa Iran.
