Leo ni Jumanne 11 Mfunguo Saba Rabiuthani 1446 Hijria mwafaka na tarehe 15 Oktoba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1226 iliyopita, alifariki dunia Abu Ali Khayyat, mnajimu na mtaalamu wa hesabati wa Kiislamu. Abu Ali ni mmoja wa shakhsia aliyekuwa na nafasi kubwa wakati wake huku jina lake likiwekwa mstari wa mbele katika kitabu cha majina ya wasomi wakubwa na mashuhuri wa dunia.
Msomi huyo ameandika vitabu vingi maarufu zaidi kikiwa ni kitabu cha ‘Mawaalid’ na ‘Siyarul-A’amaal.’ Vitabu vingi vya Abu Ali Khayyat vimetarjumiwa kwa lugha ya Kilatini.

Siku kama ya leo miaka 838 iliyopita, alizawa mjini Mosul, moja ya miji mashuhuri ya Iraq, Ibn Khallikan, kadhi, mwanahistoria na mtaalamu wa fasihi wa Kiislamu.
Akiwa kijana alisoma elimu za awali katika mji alikozaliwa na kisha kufanya safari mbalimbali na kukutana na wanasheria wa Kiislamu na wanahistoria wakubwa sanjari na kustafidi na elimu kutoka kwao. Kwa muda mrefu Ibn Khallikan alikuwa kadhi mjini Damascus, Syria ya leo huku akiwa mtaalamu pia katika elimu za historia, fasihi ya Kiarabu na mashairi.
Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia mwezi wa Rajab mwaka 681 Hijiria baada ya kuugua na kuzikwa chini ya mlima Qasioun ulio Damascus ambako pia wamezikwa wasomi wengi. Kitabu muhimu zaidi cha Ibn Khallekan ni Wafayatul A’yan.

Katika siku kama ya leo miaka 180 iliyopita alizaliwa mwanafalsafa wa Kijerumani Friedrich Wilhelm Nietzsche.
Baada ya kuhitimu masomo, Nietzsche alianza kufunza katika Chuo Kikuu cha Basel. Mwanafalsafa huyo alikuwa akipinga dini na misingi ya kimaadili na katika falsafa na mitazamo yake alikuwa akiamini nadharia ya “Superman”, kwa maana ya mtu mwenye uwezo kupita kiasi. Nietzsche alikuwa akiamini kwamba, mtu mwenye uwezo kupita kiasi au Superman ni matokeo ya irada na matashi ya mwanadamu na huwa juu ya mema na mabaya yote.
Mwanafalsafa huyo ameandika vitabu kadhaa ikiwa ni pamoja na Beyond Good and Evil, The Birth of Tragedy na Thus Spoke Zarathustra. Katika kipindi cha mwishoni mwa uhai wake Friedrich Wilhelm Nietzsche alipoteza mlingano wa kifikra na alifariki dunia mwaka 1900.

Tarehe 24 Mehr miaka 46 iliyopita, kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuwaenzi na kuwakumbuka mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran.
Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.

Miaka 33 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Bosnia Herzegovina ilijitangazia uhuru kutoka kwa Yugoslavia. Jamhuri ya Bosnia Herzegovina kijiografia ipo kusini mwa baara Ulaya na inapakana na nchi za Croatia na Yugoslavia.
Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia Bosnia Herzegovina iliunganishwa na nchi ya Yugoslavia. Bosnia Herzegovina kama zilivyokuwa nchi zingine kama Serbia, Croatia, Slovenia na nyinginezo nayo ilipagania uhuru na kufanikiwa kujikomboa katika siku kama aya leo.

Na leo tarehe 15 Oktoba ni Siku ya Vipofu Duniani.
Suala la usalama wa vipofu na haki zao za kijamii daima lilikuwa likipewa umuhimu maalumu katika jumuiya za kimataifa na kwa msingi huo mwaka 1950 Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) na Baraza la Kimataifa la Vipofu zilikutana na kupasisha sheria ya Fimbo Nyeupe na kuitangaza tarehe 15 Oktoba kuwa ni Siku ya Fimbo Nyeupe au Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Vipovu.
Miongoni mwa vipengee vya sheria hiyo ni pamoja na haki ya vipofu kutumia suhula zote za hali bora ya kimaisha katika jamii, kuwahamasisha watu wa jamii hiyo kushiriki katika masuala ya serikali na kupewa ajira serikalini, kulinda haki za vipofu wakati wa kuvuka barabara na kadhalika.
