Leo ni Jumanne tarehe 17 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 19 Novemba 2024.
Siku kama ya leo miaka 1155 iliyopita, alifariki dunia Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab, msomi mashuhuri wa lugha na nahau.
Tha’labi aliyekuwa na asili ya Iran ya alizaliwa mwaka 200 Hijiria mjini Baghdad. Kutokana na kumbukumbu yake nzuri alijifunza kwa haraka elimu ya nahau, lugha ya Kiarabu, kusoma Qur’ani na hadithi mbele ya walimu wa zama hizo. Akiwa kijana mdogo tayari alikuwa amehifadhi fasihi ya lugha ya Kiarabu ambapo alilipa umuhimu suala hilo huku akifikia daraja ya juu katika uga huo.
Miongoni mwa athari zilizosalia hii leo kutoka kwa Abul-Abbas Ahmad Ibn Yahya Tha’lab ni kitabu cha ‘Majaalisu Tha’lab’ ‘Kitabul-Faswiih’ na ‘Qawaidu al-Shi’r.’

Miaka 996 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa mmoja wa wasomi na wanafalsafa wakubwa wa Kiislamu na Kiirani, Abu Hamid Muhammad Ghazali, maarufu kwa jina la Imam Muhammad Ghazali.
Ghazali alisoma elimu ya fiq’hi kutoka kwa Abu Nasri Ismail na baada ya kufikia umri wa miaka 28 alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa Kiislamu katika elimu hiyo.
Umaarufu wa Imam Muhammad Ghazali ulipelekea kiongozi wa Iraq wakati huo Khoja Nidham al-Mulk kumwalika msomi huyo kwenda mjini Baghdad kwa ajili ya kufundisha. Hatimaye alirejea Iran na kujishughulisha na masuala ya ualimu.
Kabla ya kurejea Iran, Imam Muhammad Ghazali alipata kuandika vitabu vya thamani kama “Ihyau Ulumuddin,” “Kemia ya Saada” na “Nasaha za Wafalme”.

Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita, alifariki dunia Franz Schubert mtunzi wa nyimbo maarufu wa nchini Austria. Schubert alizaliwa mwaka 1797 katika familia masikini.
Tangu akiwa kijana mdogo alipendelea sana nyimbo huku akiwa na kipawa kikubwa katika uwanja huo na hivyo kuamua kusomea taaluma hiyo.
Alianza kubuni nyimbo akiwa kijana na katika umri wake wote aliimba zaidi ya nyimbo 600. Hata hivyo licha ya kuimba nyimbo nyingi hususan mziki wa asili, bado hakuweza kujinasua kutoka kwenye umasikini. Hii ni kwa kuwa nyimbo zake hazikupokelewa kwa wingi na jamii ya wakati wake. Ni baada ya kufariki dunia ndipo nyimbo zake zikapewa umuhimu mkubwa katika jamii.

Miaka 107 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko Allahabad nchini India, Bi Indira Gandhi binti pekee wa Jawaharlal Nehru. Mwaka 1947 baada ya India kupata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza na baba yake kuwa Waziri Mkuu wa India, Indira Gandhi alikuwa na nafasi muhimu kando ya baba yake. Mwaka 1964 baada ya kufariki dunia baba yake, Indira Gandhi aliteuliwa katika serikali ya Lal Bahadur Shastri kuwa Waziri wa Habari, Radio na Televisheni. Bi Indira Gandhi alikuwa Waziri Mkuu wa India kuanzia mwaka 1966 hadi 1984 alipouawa.

Katika siku kama ya leo miaka 47 iliyopita, Anwar Sadat Rais wa wakati huo wa Misri alifanya safari katika Baitul Muqaddas huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Hiyo ilikuwa safari ya kwanza kufanywa na Rais wa nchi ya Kiarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu. Safari hiyo ilifanyika katika fremu ya kujikurubisha Misri kwa utawala haramu wa Israel. Safari ya Anwar Sadat iliwakasirisha mno Waislamu hasa wananchi wa Palestina. Licha ya hali hiyo mwaka 1978 Anwar Sadat alitiliana saini mkataba wa Camp David na utawala huo ghasibu kwa usimamizi wa Marekani. Nchi nyingi za Kiarabu na baadhi ya nchi za Kiislamu zilikata uhusiano na serikali ya Misri zikionyesha kuchukizwa na hatua hiyo ya Sadat ambayo pia ilizusha machafuko na ghasia nchini Misri kwenyewe.
Hatimaye mwaka 1981 Khalid Islambuli aliyekuwa afisa katika jeshi la Misri alimpiga risasi na kumuua Sadat akipinga hatua yake ya kutia saini mkataba muovu wa Camp David.
