Leo ni Jumamosi 7 Mfunguo Nane Jamadul-Awwal 1446 Hijria mwafaka na 9 Novemba 2024 Miladia.
Katika siku kama hii ya leo tarehe 7 Jamadil Awwal miaka 1057 iliyopita aliaga dunia qari na mtaalamu maarufu wa Hadithi Ibn Ghalbun. Msomi huyo wa Kiislamu alizaliwa mwaka 309 Hijria katika mji wa Halab (Aleppo) nchini Syria lakini akachaga maskani nchini Misri. Ibn Ghalbun alijifunza qira ya Qur’ani na Hadithi kwa wanazuoni wa zama zake na kuwa mwalimu mahiri katika taaluma hizo. Mtaalamu huyo wa Hadithi wa Kiislamu alikuwa ya mitazamo mipya kuhusiana na elimu ya qiraa ya Qur’ani tukufu ambayo imeelezwa na mwanafunzi wake, Makki bin Abu Twalib katika kitabu cha al Kashf. Vilevile alikuwa hodari na gwiji katika fasihi na mashairi ya lugha ya Kiarabu. Kitabu muhimu zaidi ya Ibn Ghalbun ni al Irshad kinachohusiana na visomo saba vya Qur’ani tukufu.

Siku kama ya leo miaka 206 iliyopita, alizaliwa Ivan Turgenev mwandishi mashuhuri wa riwaya wa Russia. Turgenev alisomea fasihi ambapo vitabu vyake vingi vilitetea sana uhuru na haki za wanavijiji. ni kutokana na sababu hiyo ndio maana alisumbuliwa na utawala wa Kitzar wa Urusi na kuulazimika kuhama na kuuelekea Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, alizaliwa nchini Pakistan Allama Muhammad Iqbal Lahori mwandishi, mwanafikra na malenga mzungumza lugha ya Kifarsi. Baada ya kumaliza masomo yake ya juu, Iqbal Lahori alielekea katika nchi za Ujerumani na Uingereza kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu zaidi katika taaluma ya falsafa. Alianza kusoma mashairi akiwa kijana na shairi lake la kwanza alilipa jina la ‘Naleh Yatiim’ kwa maana ya kilio cha yatima. Allama Iqbal Lahori alikuwa mwanaharakati pia aliyepambana kwa minajili ya kuikomboa Pakistan kutoka mikononi mwa India. Allamah Muhammad Iqbal alifariki dunia mwaka 1938.

Miaka 106 iliyopita sawa na tarehe 9 Novemba mwaka 1918, mfumo wa jamhuri ulitangazwa huko Ujerumani kufuatia kushindwa mara kadhaa jeshi la nchi hiyo na vikosi vya Waitifaki katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kuzuka uasi nchini humo. Matukio hayo yalipelekea kujiuzulu Wilhelm wa Pili mtawala wa mwisho wa kifalme wa nchi hiyo. Siku mbili baadaye mfalme huyo alikimbilia Uholanzi na hivyo utawala wa kifalme ukawa umehitimishwa nchini Ujerumani. Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita vya Kwanza vya Dunia na kufutwa utawala wa kifalme, Friedrich Ebert alishika madaraka ya nchi kama rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Abdul Aziz bin Saud mfalme wa kwanza wa Saudi Arabia na mwasisi wa utawala wa Aal Saud. Abdul Aziz bin Saud ambaye ni mwasisi wa utawala wa kifamilia wa Saudi Arabia, alizaliwa tarehe 15 Mei 1880. Mtawala huyo alikuwa kibaraka wa Uingereza na tangu awali alikuwa na tamaa ya kutawala nchini Saudi Arabia hususan katika maeneo matakatifu ya Makka na Madina.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, nchi ya Cambodia ilijikomboa kutoka kwenye makucha ya mkoloni Mfaransa na kujitangazia uhuru. Kijiografia Cambodia ipo kusini mashariki mwa Asia. Akthari ya wananchi wa Cambodia ni wa jamii ya Khmer na wanazungumza lugha ya Kikhmeri. Kuanzia karne ya 8 hadi 13 Miladia, Cambodia ilikuwa nchi yenye nguvu ambapo mbali na ardhi ya sasa ya nchi hiyo, sehemu kubwa ya ardhi ya Thailand, Laos na Vietnam ilikuwa katika udhibiti wa nchi hiyo.

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita Dakta Sayyid Hussein Fatimi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Muhammad Musaddiq, aliuawa kwa kupigwa risasi na vibaraka wa utawala wa Shah nchini Iran. Dakta Fatimi kabla ya hapo alikuwa amehukumiwa kunyongwa na mahakama moja ya kijeshi ya kimaonyesho ya utawala wa Shah huku akiwa mgonjwa sana. Baada ya mapinduzi yaliyofanywa na Marekani tarehe 28 Mordad mwaka 1332 Hijria Shamsiya hapa nchini Iran na baada ya kujiuzulu Dakta Musaddiq, Dakta Sayyid Hussein Fatimi alikuwa akisakwa na vibaraka wa utawala wa Shah na alikuwa akiishi mafichoni. Alikamatwa na kunyongwa katika siku kama ya leo.

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, mwanajeshi, mwanasiasa mashuhuri na rais wa zamani wa Ufaransa aliaga dunia. Jenerali Charles André Joseph Marie de Gaulle alizaliwa Novemba 22 mwaka 1890 katika mji wa Lille. Mwaka 1940 aliteuliwa kuwa jenerali kijana zaidi katika Wizara ya Ulinzi ya Ufaransa. Baada ya majeshi ya Ufaransa kushindwa na Ujerumani katika vita, Charles de Guelle alikimbilia Uingereza na kuongoza harakati za mapambano ya Ufaransa.

Katika siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, ukuta wa Berlin ambao ulikuwa ukiugawa mji huo katika sehemu mbili za mashariki na magharibi kwa kipindi cha miaka 28 hatimaye ulivunjwa. Baada ya Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa mji huo lilikuwa likidhibitiwa na Urusi ya zamani, huku eneo la magharibi likidhibitiwa na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Machafuko yaliyotokea mjini Berlin hapo mwaka 1961 na wakazi wa mashariki kukimbilia upande wa magharibi, kulizitia wasiwasi serikali za Urusi ya zamani na Ujerumani Mashariki, suala lililozipelekea nchi hizo kujenga ukuta huo ambao baadaye uliokana kuwa nembo ya kuwaganywa Ujerumani. Hata hivyo kuporomoka kwa Urusi ya zamani ambako kuliacha taathira kubwa katika tawala za kikomunisti za Ulaya Mashariki kulipelekea kuvunjwa ukuta huo wa Berlin hapo mwaka 1989.
