
KIPA wa kimataifa wa Tanzania anayewanoa makipa wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amekabidhiwa mikoba ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Melis Medo ambaye ametimkia Singida Black Stars.
Februari 25, Kagera Sugar iliachana na Medo baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na sasa wapo katika hatua za mwisho kumalizana na Kaseja, ili aweze kuisaidia timu hiyo kumaliza msimu bila kushuka daraja.
Chanzo cha kuaminika kutoka Kagera, kimeliambia Mwanaspoti uongozi umeamua kumpa timu Kaseja kutokana na uzoefu alionao katika ligi hiyo na anaifahamu vizuri timu na mazingira yake, hivyo wanaamini ataweza kuivusha ilipo kwenda hatua nyingine.
Kaseja ambaye anakubalika zaidi na mabosi wa Kagera kutokana na kujitolea kwake katika kikosi, wanaamini ataweza kuwajenga wachezaji waliopo na kuwapa nguvu ya kuipambania timu isishuke daraja.
“Tumebakiza mechi chache na tuna mtu ambaye ni mkonge na amekuwa na maelewano mazuri na wachezaji, tumepanga kumtumia yeye kuipambania timu isishuke ni mchezaji kiongozi hivyo atawaongoza vijana kupambana,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Kaseja amejenga uaminifu mkubwa ndani ya timu. Amekuwa chachu ya mafanikio katika timu na anautumia vizuri uzoefu wake katika kuwaongoza vijana.”
Chanzo hicho kimesema Kaseja atasaidiana na Temmy Felix na Paul Ngwai kuhakikisha timu hiyo inasalia Ligi Kuu Bara msimu ujao, kwani sasa ipo nafasi ya 15, ikiwa na pointi 16 baada ya mechi 22.