Juma Choki: Mbabe mwenye kwenye ndondi

Juma Ramadhani Choki, mtoto wa mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar na Singida Big Stars, Ramadhan Choki ambaye huenda jina lake likaandikwa kwa wino wa dhahabu, mwaka huu.

Wakati baba yake alifanikiwa kutamba katika mchezo wa soka lakini kijana wake amekuwa moto wa kuotea mbali katika mchezo wa ngumi za kulipwa huku akiweka rekodi mbalimbali ikiwemo kumpiga kwa majaji watatu bondia aliyekuwa akimvutia siku zote, Nasibu Ramadhan ‘Pacman’.

Choki mwenye rekodi ya kucheza jumla ya mapambano kumi, ameshinda tisa kati ya hayo matatu ameshinda kwa Knockout na moja akiwa ametoka sare na hajawahi kupoteza pambano lolote katika ngumi za kulipwa.

Bondia huyo katika mabondia bora wa Tanzania yaani ‘Pound for  Pound’ anakamata nafasi ya nane lakini katika mabondia bora wa uzani wake wa super feather anakamata nafasi pili katika mabondia 91 wakati duniani akiwa 100 katika mabondia 1960 huku akiwa na hadhi ya nyota mbili na nusu.

Choki ambaye alianza ngumi za kulipwa mwaka 2017, wikiendi iliopita ameipa Tanzania habari njema kutokana na kuwa bondia pekee wa ngumi za kulipwa nchini kuchaguliwa kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia la Ngumi ambayo yanaratibiwa na Baraza la Ngumi Duniani WBC kupitia mpango wa Riyadh Season Grandprix chini ya Familia ya Kifalme ya Saudi Arabia.

Bondia huyo amefanya mahojiano maalumu Mwananchi juu ya yeye kuweza kuchaguliwa huku akiwa bondia pekee kutoka Tanzania kuwepo kwenye orodha ya mabondia 128 kutoka duniani kote.

“Kuhusu kuwepo kwenye Grandprix, huu mchongo ulianzia kwenye menejimenti ambayo inanisimamia ya AAM Seddiqi chini ya bosi wangu Ahmed Abdul Mageid Seddiq ambayo ipo nchini Dubai.

“Kabla wao walinipa taarifa kwamba jina langu wanalipeleka kwenye WBC Grandprix huko Saudi Arabia na baada ya jina langu kurudi ndiyo wakanipa mchoro kwamba natakiwa kucheza kwenye uzani wa feather ingawa madaraja ya uzani yatakuwa tofauti.

“Lakini pia mpaka kufikia kucheza fainali natakiwa kucheza mapambano manne na kila pambano nikicheza nitakuwa napewa mwezi mmoja wa kujiandaa na pambano lingine.

“Kuhusu tarehe au lini mashindano yataanza kiukweli bado hajasema  lakini nadhani huenda mashindano yakaanza mwezi ujao.”

Baada ya taarifa kutoka, Kamisheni ya Ngumi Tanzania imekutafuta?

“ TPBRC niliwatafuta kwa hekima yangu kwa sababu ni jambo kubwa na lishakuwa la kitaifa hivyo siwezi kulibeba mwenyewe, nilimpigia makamu mwenyekiti, Alex Galinoma, nilimueleza kwamba nimeweza kuchaguliwa kushiriki mashindano ya WBC Grandpix.

“Galinoma aliniambia sawa na ameona lakini alinishukuru kwa kuweza kuwapa taarifa na akaniuliza nahitaji kitu gani, nikamwambia nahitaji sapoti yao kama kijana wao, bondia wao wa Tanzania.

“Lakini kama bondia chipukuzi, naenda kulipambania taifa langu la Tanzania kwa hiyo mimi naomba serikali yangu ya Tanzania iweze kusapoti hili jambo kwa kuwa ni la kitaifa siyo jambo dogo.

“Kupitia kamisheni yangu TPBRC, waweze kunisapoti, viongozi wa serikali waweze kujua tunalifanyaje hili jambo, naomba sapoti yao ya aina yoyote  ikiwemo kupata vifaa, maandalizi kwa sababu nahisi mashindano ni mwezi wa nne.”

Wakati mnasubiri kupata sapoti, kambi umepanga kuweka wapi?

“Bado sijajua kwakweli ingawa nimeongea na menejimenti yangu huenda nikaenda kuweka Dubai, Mungu akipenda ila kwa sasa naendelea na maandalizi ya ndani chini ya waalimu wangu ambao nao natamani kwenda nao kwenye kambi yangu kabla mashindano.”

Pambano gani kwako lilikuwa gumu?

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 2020 dhidi ya Emmanuel Mwakyembe kwa sababu ilikuwa ni pambano la marudiano baada ya kumchapa kwenye pambano la King of the Ring, pambano lilikuwa gumu kweli lakini nashukuru Mungu nilishinda.

Kitu gani ulishawahi kukutana nacho katika ngumi kikatisha tamaa?

“Nakumbuka nilishiriki mashindano ya King of the Ring, mwaka 2018 na nikafanikiwa kuibuka mshindi katika pambano la fainali niliibuka kuwa bingwa.

“Lakini kwa matokeo yaliyotokea ambayo nilishinda na Watanzania wakajua kuwa nimechukua King of the Ring na bahati nzuri walitoa zawadi pale.

“Nilipewa zawadi ya pikipiki lakini ilikuwa siyo haki kwa sababu waliweka pikipiki ambayo ilikuwa mbovu ambayo ishatumika mwaka mmoja na miezi sita, yaani kama walinidhulumu kiasi fulani.

“Kiukweli ilinitoa sana kwenye reli, ilinichanganya kisaikolojia kwa sababu hata nilivyorejea mtaani, watu walikuwa wanasema nimepewa zawadi ya pikipiki mbovu.

“Binafsi hiyo kitu hainitoki katika moyo wangu na ndiyo inanifanya  nakuwa na juhudi sana ya mazoezi,” alisema Choki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *