Julio ashtukia jambo Kiluvya United

KOCHA mpya wa Kiluvya United, Julio Elieza amesema kwa nafasi iliyopo timu hiyo kwa sasa bado haiwapi kiburi cha kuamini moja kwa moja kama watabakia kwa msimu ujao, hivyo anapambania kuhakikisha malengo aliyoyapewa na uongozi anayatimiza.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Julio alisema gepu la pointi lililopo na washindani wao waliokuwa chini linaonyesha hawako sehemu salama, hivyo jitihada zinahitajika ili kukinusuru kikosi hicho na janga la kushuka daraja.

“Hatuwezi kujihakikishia moja kwa moja sisi tutabaki kwa sababu hayo ndiyo malengo niliyopewa na uongozi, tuna kazi ya kufanya kwa michezo hii ya mwishoni ambayo huwa ni migumu kutokana na mahitaji ya kila mmoja wetu kwa sasa,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli FC ya Iringa, alisema ili kufikia malengo hayo ni lazima apate ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na wachezaji kijumla, kwani hiyo ndio itakayokuwa silaha kubwa ya kufikia na kutimiza kule wanapopahitaji.

Julio anakuwa ni kocha wa tatu msimu huu kuiongoza timu hiyo baada ya awali kufundishwa na Twaha Beimbaya aliyetimuliwa kutokana na matokeo mabaya, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Zulkifri Iddi ‘Mahdi’ ambaye pia ameondoka kikosini humo.

Kikosi hicho kilichopanda Ligi ya Championship msimu huu, kimecheza michezo 24 hadi sasa na kati ya hiyo kimeshinda sita, sare mmoja na kuchapwa 17, kikishika nafasi ya 12 na pointi 19, huku kikifunga jumla ya mabao 17 na kuruhusu 37.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *